Tangazo La Kuwarejesha Wagombea Wasio Na Makosa Ya Kikanuni Kwenye Uchaguzi Wa Serikali Za Mitaa 2019

Zoezi la Uchukuaji fomu, Urudishaji fomu, Uteuzi, Pingamizi na Rufaa lilianza tarehe 29/10/2019 na kumalizika tarehe 9/11/2019.
 
Katika zoezi hilo jumla ya wananchi 555,036 kutoka Vyama mbalimbali vya Siasa walifanikiwa kuchukua fomu za kugombea. Na jumla ya wananchi 539,993 sawa na asilimia 97.3 walifanikiwa kurejesha fomu.
 
Wagombea kutoka Chama cha Mapinduzi waliochukua fomu walikuwa 412,872 (asilimia 74), Chama cha Demokrasia na Maendeleo walikuwa 105,937 (asilimia 19), Chama cha Wananchi CUF walikuwa 24,592 (asilimia 4), ACT Wazalendo walikuwa 8,526 (asilimia 1.5), NCCR – Mageuzi walikuwa 2,244 (asilimia 0.4) na Vyama vingine vyenye usajili
wa kudumu walichukua chini ya asilimia 0.1 kwa kila chama.
 
Katika zoezi zima la kuchukua na kurejesha fomu kulikuwa na changamoto kubwa kwa wagombea wengi kufanya makosa mengi ya kikanuni yaliyopelekea wengi wao kutoteuliwa. 

Baadhi ya makosa hayo ni pamoja na kujidhamini wenyewe, kutojaza fomu namba IV, kutofautiana kwa majina, kutojaza fomu kwa ukamilifu, kuandika umri, kukosea umri (mfano amezaliwa mwaka 2019) na makosa mengine mengi mbalimbali. Hii ilitokana na baadhi ya vyama kushindwa kuwajibika ipasavyo katika kuwaelekeza wanachama wao. Kutokana na hali hiyo pingamizi na rufaa mbalimbali zipatazo 15,380 ziliwasilishwa.
 
Hadi zoezi la maamuzi ya rufaa mbalimbali lilipohitimishwa tarehe 9/11/2019, jumla ya rufaa 4,921 (32%) zilipitishwa na zilizobaki zilikosa sifa kwa sababu mbalimbali.
 
Katika mchakato huo wa kuchukua na kurudisha fomu Chama cha Mapinduzi kimefanikiwa kupita bila kupingwa katika maeneo mbalimbali kwakuwa hapakuwa na mgombea yoyote kutoka Chama cha Upinzani. Kwa upande wa Wenyeviti wa Vijiji Chama cha Mapinduzi kimepita bila kupingwa katika vijiji 6,248 kati ya vijiji 12,319 sawa na asilimia 51. 

Kwa upande wa Mitaa Chama cha Mapinduzi kimepita bila kupingwa katika Mitaa 1,169 kati ya Mitaa 4,263 sawa na asilimia 27 Kwa upande wa Vitongoji Chama cha Mapinduzi kimepita bila kupingwa katika Vitongoji 37,505 kati ya Vitongoji 64,384 sawa na asilimia 58. Kwa upande wa Wajumbe wa kundi la wanawake jumla ya wajumbe 64,085 wamepita bila kupingwa na wajumbe kundi mchanganyiko jumla ya wajumbe 75,560 wamepita bila kupingwa.
 
Kwa kuwa imeonekana wazi wananchi kutoka vyama mbalimbali wamekuwa na nia kubwa ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi licha ya vyama vyao kutokuweka umuhimu katika kuwaelekeza vyema wanachama wao juu ya ujazaji fomu kwa mujibu wa Kanuni. 

Mamlaka ya Uchaguzi imeona ni vyema wananchi hao kupewa nafasi ya kushiriki katika Uchaguzi kwani imejidhihirisha wazi hata baada ya vyama viwili vilivyojitoa bado wanachama wao waliendelea kuwasilisha rufaa zao ili wapewe nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.
 
Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019 Tangazo la Serikali Na. 371 la Mwaka 2019 Kanuni ya 49, Tangazo la Serikali Na. 372 la Mwaka 2019 Kanuni ya 51, Tangazo la Serikali Na. 373 la Mwaka 2019 Kanuni ya 52, na Tangazo la Serikali Na. 374 la Mwaka 2019 Kanuni ya 52 ninatoa muongozo kwamba Wagombea wote ambao walioteuliwa na kudhaminiwa na vyama vyao na kufanikiwa kurejesha fomu zao za uteuzi kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika kipindi kilichokuwa kimepangwa cha kuchukua na kurejesha fomu kilichoanza tarehe 29*/10/2019 na kumalizika tarehe 04/11/2019 kwa Tangazo hili wanapewa sifa ya kupigiwa kura na wananchi wa Kijiji, Mtaa, au Kitongoji husika kwa ajili ya Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019 isipokuwa tu kama atakuwa amekutwa na mambo yafuatayo:
 
1. Siyo Raia wa Tanzania,
2. Hajajiandikisha katika Kijiji, Mtaa, au Kitongoji husika,
3. Amejiandikisha mara mbili,
4. Amejidhamini Mwenyewe,
5. Hajadhaminiwa na chama chake cha Siasa,
6. Wamerejesha fomu watu zaidi ya mmoja kutoka chama kimoja kwa nafasi inayofanana ya Mwenyekiti wa Kijiji, Mtaa, au Kitongoji kwa Kijiji, Mtaa, au Kitongoji husika. Msimamizi Msaidizi hata wajumuisha wagombea hao katika orodha ya wanaopaswa kupigiwa kura,
7. Amejitoa kwa mujibu wa Kanuzi za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tangazo la Serikali Na. 371 la Mwaka 2019 Kanuni ya 19, Tangazo la Serikali Na. 372 la Mwaka 2019 Kanuni ya 20, Tangazo la Serikali Na. 373 la Mwaka 2019 Kanuni ya 20, na Tangazo la Serikali Na. 374 la Mwaka 2019 Kanuni ya 20.
 
Msimamizi wa Uchaguzi ataanza kupokea ratiba za kampeni kutoka katika Vyama vya Siasa kuanzia leo hii tarehe 10/11/2019 hadi kesho jioni kwa ajili ya kuziunganisha.
 
Tarehe ya matukio na shughuli zingine zote zinazohusu Uchaguzi huu zitaendelea kwa mujibu wa Kanuzi za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2019.
 
Selemani S. Jafo (Mb.)
WAZIRI WA NCHI – TAMISEMI
10 Novemba, 2019

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post