SERIKALI YASEMA IMEJIPANGA KUDHIBITI SUMU KUVU, KIWANDA CHA A TO Z KUANZA KUZALISHA KIDHIBITI CHA SUMU HIYO 'AFLASAFE' NA KUKISAMBAZA KWA WAKULIMA


Na Seif Mangwangi, Arusha

KIWANDA Cha A to Z cha Jijini hapa kimesema kiko kwenye taratibu za mwisho za kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha kiuatilifu aina ya Aflasafe kwaajili ya kuzuia maambukizi ya sumukuvu ambayo inaelezwa kusababisha madhara makubwa kwa afya za binaadam ikiwemo saratani ya ini.
 
wajumbe wa mkutano wakiwa katika picha ya pamoja na waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wa tano aliyekaa mbele

Mtendaji mkuu wa kiwanda cha A to Z, Kalpesh Shah amesema tangu walipoingia mkataba na taasisi ya  Kimataifa ya International Institute for Transforming African Agriculture (IITA), kutengeneza kiuatilifu hicho (Aflasafe), tayari wameshawekeza mtaji wa dola za Kimarekani milioni 0.35 na matarajio ni kutumia dola milioni 1.5 katika miaka mitano ijayo.

Akiwasilisha mada kwenye mkutano wa kwanza wa Afrika wa kudhibiti Sumukuvu (Aflasafe) kwenye vyakula unaoendelea kwa siku yake ya mwisho leo jijini hapa, Kalpesh Shah amesema sumu kuvu ni ngumu sana kuitambua kwenye mazao hivyo zinahitajika gharama kubwa sana kukabiliana nayo.

Amesema A to Z kupitia taasisi yake ya Africa Research Institute wanayoiendesha kwa ushirikiano na Sumitomo, imekuwa ikipambana kufanya tafiti mbalimbali na kuja na teknolojia mbadala ya kupambana na magonjwa tofauti athari kwa binaadam ikiwemo kutengeneza chandarua chenye kiuatilifu cha kuua mbu wanaoenea ugonjwa wa malaria lakini pia mifuko ya kuhifadhi mazao yasiweze kuharibiwa na wadudu waharibifu.

Akifungua mkutano huo wa Kimataifa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema Serikali imedhamiria kukabiliana na sumukuvu kwa kuanzisha tafiti katika mazao ambayo yanaelezwa kukumbwa na ugonjwa huo ikiwemo mahindi na karanga.
 
Washiriki wa mkutano huo wakiwa katika picha ya pamoja
Amesema katika kuonyesha nia ya kukabiliana na tatizo hilo,  hivi karibuni, Serikali ya Tanzania ilipata fedha za kutekeleza mradi wa kuzuia kuenea kwa sumukuvu hapa nchini (TANIPAC).

Waziri Hasunga amesema lengo la Serikali ni kupunguza kutokea kwa madhara ya sumukuvu katika mfumo wa chakula kupitia udhibiti husishi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya mahindi na karanga, hivyo kuboresha uhakika na usalama wa chakula na hatimae kuimarisha afya na lishe ya jamii yetu na kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi zinazotuzunguka.

Mkakati huo unazingatia udhibiti wa sumukuvu katika hatua za uzalishaji, uvunaji, udhibiti wa kibaolojia, teknolojia baada ya kuvuna na njia za ukaushaji, uhifadhi, kujenga uwezo wa kitaasisi, uratibu na kutoa elimu ya kuhamasisha wadau muhimu. Ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu katika uhaulishaji wa teknolojia pamoja na kuhakikisha mradi unakuwa endelevu.


Waziri Hasunga amesema kuwa Ushirikiano wa kiutafiti, kati ya sekta binafsi na watunga sera, ni muhimu katika kufanikisha mageuzi ya kilimo.

Amesema tangu kuibuka kwa tatizo la sumukuvu mwaka 2016, Tanzania imechukua hatua mbalimbali za kupunguza kusambaa kwa sumukuvu hapa nchini kwa kutambua changamoto za kukabili sumukuvu, ambapo kunahitajika kutumia njia mbalimbali kuanzia kwenye hatua za uzalishaji, uvunaji, uhifadhi, usindikaji na kuhusisha sekta za Umma na Binafsi katika kupunguza upotevu wa chakula na kuongeza upatikanaji wa chakula salama na lishe bora.

Amesema, Tanzania imeanzisha Kamati  Jumuishi ya Uendeshaji inayohusisha sekta na taaluma kutoka taasisi mbalimbali chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Kilimo ambayo ina mamlaka ya kusimamia masuala yote yanayohusu sumukuvu.

Kadhalika, amewahakikishia washiriki hao kuwa kinga ya sumukuvu - Aflasafe TZ01;  imeshasajiliwa kwa matumizi hapa nchini Tanzania na kampuni iliyopewa jukumu la kuendesha mradi huo ni kiwanda cha A to Z kilichokuwepo kisongo jijini Arusha. 

 "Aidha, nimefarijika kuwa kazi hii inafanywa na Kampuni Binafsi ambayo imewekeza katika uzalishaji, na usambazaji wa bidhaa hii ambayo itaokoa Maisha ya watu hapa nchini, A to Z ni kiwanda kikubwa na nina uhakika kazi hii wataifanya vizuri sana," Alisisitiza

"Napenda kuwahakikishia utayari wa Wizara yangu katika kuyatumia maazimio mtakayokubaliana katika mkutano huu. Aidha, Serikali ya Tanzania, inatilia maanani na inaunga mkono hatua zinazochukuliwa katika kuhimiza biashara ya chakula salama, usalama wa chakula na lishe" Alisema Waziri Hasunga

Tanzania kwa sasa inatekeleza Awamu ya Pili ya  Programu ya Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo (ASDP II) yenye lengo la kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo kuwa na kilimo chenye tija na kibiashara, pamoja na kukuza uchumi wa wakulima wadogo na kuboresha maisha, uhakika wa chakula na lishe bora.

Uhakika wa chakula na lishe ni muhimili ambao ni muhimu wa ASDP II Katika kufikia malengo hayo, uwekezaji katika utafiti wa kilimo ni muhimu katika kuleta matokeo kwa wakulima na wadua wengine katika mnyororo wa thamani.

Waziri Hasunga amesema kuwa kutokana na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) za mwaka 2017, Tanzania inaongoza katika uzalishaji wa mahindi na karanga katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki, kwa kuzalisha tani milioni 6 na tani milioni moja mtawalia.

Amesema, Pamoja na mafanikio hayo, Serikali inatambua kuwa, ingawa mazao hayo ni muhimu kwa chakula cha kila siku, lakini yanakabiliwa na ukubwa wa tatizo la sumukuvu ambalo linahatarisha usalama wa chakula na kuwa kikwazo cha biashara ya mazao hayo kwa nchi jirani na Tanzania.

Mkutano huu ambao umewaweka pamoja watafiti, wafanyabiashara, watunga sera na wadau wa maendeleo, ambao unalenga kupanga mikakati ya kuongeza kasi ya matumizi ya kinga ya sumukuvu (Aflasafe), na kukabili sumukuvu barani Afrika, unadhihirisha mabadiliko chanya ya kimtazamo tunayoyahitaji.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post