SEKTA YA NGOZI, NYAMA NA MAZIWA ZAUNDIWA KOZI FUPI VYUONI

Na. Edward Kondela

Serikali imewataka wadau kwenye sekta ya ngozi, nyama na maziwa wanaoandaa mitaala kwa ajili ya vyuo kufundisha kozi fupi katika sekta hizo ngazi ya cheti na diploma kupitisha mitaala bora itakayohakikisha wanafunzi watakaohitimu mafunzo wanaleta matokeo chanya katika sekta hizo kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Akizungumza Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kilichowahusisha wadau katika sekta za ngozi, nyama na maziwa kutoka serikalini na taasisi binafsi Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ili kupata malighafi bora zinazotokana na sekta ya ngozi, nyama na maziwa ni lazima wataalam ambao wamesomea sekta hizo ngazi ya cheti na diploma wawekewe mazingira ya kuhakikisha wanatumia utaalam watakaoupata kupitia vyuo mbalimbali baada ya kupitishwa kwa mitaala hiyo ili iwe na tija kwa taifa.

“Mitaala mnayokwenda kupitia na kuzungumzia lazima ijibu mahitaji ya wadau katika sekta tatu yaani ngozi, nyama na maziwa isiwe kuwa na cheti baada ya kuhitimu mafunzo ngazi ya cheti au diploma hawa wataalamu wa ngazi ya kati ndiyo wanaotegemewa kwenda kufanya kazi za vitendo, hakikisheni mnapata mitaala ambayo itakuwa na manufaa.” Amesema Prof. Gabriel

Aidha Prof. Gabriel amewataka wadau hao kubainisha njia bora za kufundishia mara baada ya kupitishwa kwa mitaala hiyo ili kuhakikisha wanafunzi watakaodahiliwa wanaelewa vizuri pamoja na kuwa na utaratibu mzuri wa kuwapata watu ambao wanafundishika na wawe tayari kupokea mafunzo hayo.

Akibainisha juu ya jamii kuwa na ufugaji wenye tija, katibu mkuu huyo amewaasa wadau wa mifugo wajenge utamaduni wa kuwatumia wataalam hususan wa ngazi ya kati ili waweze kufuga kisasa na kunufaika kupitia mifugo yao badala ya kufuga kwa mazoea na hatimaye kupata hasara.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafiti, Ugani na Mafunzo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa amesema mjadala wa kuandaa mitaala kwa ajili ya kufundisha vyuoni kozi fupi katika ngazi ya cheti na diploma kwenye kwenye sekta ya ngozi, nyama na maziwa umetoka kwa wadau, hivyo wizara ikashirikisha taasisi mbalimbali likiwemo Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kukamilisha mitaala hiyo.

Dkt. Mwilawa amefafanua kuwa mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kuandaa mitaala hiyo vyuo vya serikali kwa kushirikiana na binafsi vitaanza kutekeleza kwa kutoa mafunzo ya tasnia ya ngozi, nyama na maziwa katika ngazi ya cheti na diploma.

Akielezea umuhimu wa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuandaa mitaala hiyo, Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania Bw. Magembe Makoye ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuhakikisha sekta ya mifugo inasimamiwa vyema kupitia mambo ya kisera na kisheria ambayo ndiyo yamekuwa yakisimamia pamoja na kutunga kanuni mpya zenye lengo la kuhakikisha sekta ya mifugo inathaminiwa zaidi.

Bw. Makoye amesema sekta ya mifugo ambayo inaajiri watu wengi kote nchini kupitia mafunzo yatakayoanza kutolewa vyuoni mara baada ya kupitishwa kwa mitaala hiyo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza thamani ya sekta ya ngozi, nyama na maziwa kwa kuwa wafugaji sasa wataongezewa taarifa na maarifa kupitia kwa wataalamu watakaohitimu mafunzo hayo.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya ngozi, nyama na maziwa pamoja na taasisi mbalimbali likiwemo Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) inapitia mitaala kwa ajili ya kuanzishwa kwa kozi fupi ngazi ya cheti na diploma katika sekta hizo kwenye vyuo vya serikali na binafsi ili kuyaongezea thamani zaidi mazao ya ngozi, nyama na maziwa kwa kuwa na waatalamu wengi zaidi ngazi ya kati walipobobea katika sekta za ngozi, nyama na maziwa.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post