RC SINGIDA ASHAURI JESHI LA POLISI KUANZISHA DAWATI LA UPIMAJI MACHO

Mtaalamu wa macho kutoka  Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Sight Saver akimwelekeza jambo Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi wakati akimpima macho katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani uliofanyika mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick.

Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi , akipuliza kifaa cha utambuzi wa kilevi kwa dereva aliyekunywa pombe. Kulia ni Katibu Tawala wa mkoa huo, Dkt. Angelina Lutambi.
 Wananchi wakisubiri kupima macho kwenye maadhimisho hayo.
 Uandikishaji majina kabla ya kupima macho ukifanyika.
 Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi , akipata maelezo alipotembelea banda la Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Singida kwenye maadhimisho hayo.
 Uandikishaji majina kabla ya kupima macho ukifanyika.
 Mtaalamu wa macho kutoka  Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Sight Saver akimpima macho mwananchi 
 Mwanahabari wa Shirika la Habari Tanzania (TBC) Mkoa wa Singida, Leonard Manga akisoma maandishi kabla ya kupimwa macho.
 Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, akizungumza kwenye ufunguzi wa maadhimisho hayo. Kushoto ni Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida kwenye maadhimisho hayo, Afande Mwakalukwa.
 
Na Waandishi Wetu, Singida.
 
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi, ameshauri Jeshi la Polisi nchini kupitia kitengo chake cha usalama barabarani kuanzisha ‘dawati maalumu’ la upimaji wa afya ya macho ili kupunguza ajali zitokanazo na uoni hafifu.
 
Dkt. Nchimbi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mkoani hapa wakati wa zoezi la upimaji macho linaloendeshwa na Shirika lisilo la kiserkali la Sightsavers, linalokwenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya Usalama Barabarani.
 
“Kati ya dawati ambalo mnatakiwa kuwa nalo kwa sasa ni hili la afya ya macho, niwasihi shirikianeni na wataalamu wa macho nendeni mkafanye kampeni kubwa ya afya ya macho…himizeni, tuhimizeni ninyi mkisema jamii itawaelewa na ajali zote zinazotokana na tatizo hili la uoni hafifu zitapungua,” alisema Nchimbi.
 
Alisema, tunapoadhimisha wiki ya usalama barabarani tusisahau kuwa afya ya macho ni kati ya kipengele na mhimili muhimu katika suala zima la usalama barabarani hapa nchini.
 
Alieleza kuwa, endapo kila mtumiaji wa barabara atapatiwa huduma stahiki ya afya ya macho basi ni dhahiri atakuwa mwangalifu, makini na hatimaye kuweza kupiga hesabu zinazotakiwa awapo barabarani.
 
Akifafanua umuhimu wa uwapo wa dawati hilo la upimaji macho, alisema iwapo mtumiaji wa barabara anakabiliwa na tatizo la macho, mathalani wakati fulani badala ya kuona gari moja anajikuta anaona mawili au kwasababu huna uoni wa mbali una uoni wa karibu ukafikiri gari lipo karibu kumbe lipo mbali au kinyume chake, matokeo yake ni mfululizo wa matukio ya ajali kila kukicha.
 
Alisema wakati mwingine mtu yupo pembeni ya barabara lakini badala ya kusubiri anaamua kukatisha barabara akiamini chombo cha moto kilicho kulia kwake au kushoto bado kipo mbali-alisema yote hayo ni matokeo ya matatizo ya afya ya macho ambayo kwa pamoja jeshi la polisi na jamii ikiamua tatizo hilo litamalizika.
 
Dkt, Nchimbi aliongeza kuwa suala la usalama barabarani halimanishi wale wanaoendesha vyombo vya moto pekee bali ni kwa watumiaji wote wa barabara husika, ikiwemo watembea kwa miguu, na kuhimiza kila mtu anapaswa kuchukua tahadhari wakati wote.
 
“Mtumiaji wa barabara unapokuwa barabarani hakikisha kwanza macho yako yapo sawasawa, pia unapaswa kuwa wewe mwenyewe ni dereva unayejiendesha, lakini muendeshe pia na mwenzako aliye kushoto kwako, kulia kwako na nyuma yako…hii iwe kwa wote ikiwemo waendesha bodaboda, baiskeli, bajaji, wafugaji, na vyombo vingine vya moto ili tuweze kumaliza kabisa ajali hizi zinazoweza kuepukika,” alisema.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post