
Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
amezitaka halamashauri nchini kuhakikisha zinadhibiti ujenzi holela kwa
kuhakikisha utoaji vibali vya ujenzi ktika maeneo yao unazingatiwa na
kusimamiwa ipasavyo.
Dkt
Mabula alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana katika halmashauri za
wilaya za Morogoro, Mvomero pamoja na Manispaa ya Morogoro wakati wa
ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa
Morogoro.
Alisema,
halmashauri nchini zina wajibu wa kudhibiti ujenzi holela katika maeneo
mbalimbali kwa kushirikiana na Watendaji wa Mitaa na kuweka taratibu
ambazo hazitamruhusu mtu kufanya ujenzi wowote bila kupata kibali cha
ujenzi kutoka halmashauri husika.
‘’
ili kuondokana na ujenzi holela katika halmashauri zenu mwananchi
asifanye ujenzi wowote bila kupata kibali cha ujenzi kutoka halmashauri
‘’ alisema Dkt Mabula
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, zoezi la
urasimishaji linaloendelea sasa katika maeneo mbalimbali siyo zoezi la
kudumu na kulegalega kudhibiti ujenzi holela kutasababisha zoezi hilo
kutokuwa na maana kwa kuwa ujenzi holela utakuwa ukiendelea.
Akigeukia
suala la utoaji hati za ardhi, Dkt Mabula aliagiza Hati zilizokamilika
katika ofisi za Msajili wa Hati wamiliki wake watangaziwe kupitia njia
mbalimbali zikiwemo radio za Kijamii (Local Radio) sambamba na hati
hizo kutolewa kwa wamiliki wake katika eneo maalum litakaloandaliwa
karibu na maeneo wanaoishi wamiliki wa hati hizo.
Alisema,
njia ya kuwatafuta wananchi ambao hati zao zimekamilika itasaidia
kupunguza mlundikano wa Hati za Ardhi zilizokamilika kwenye Ofisi za
Msajili wa Hati tofauti na utaratibu wa sasa unaomtaka mwenye hati
kuifuata ofisi za ardhi au ile ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi za Kanda
kwenda kuchukua.
Awali
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Morogoro Patrick
Mwakilili alisema halmashauri yake imepanga kupima viwanja 1,000
kwenye makao makuu ya wilaya Mvuha na viwanja 3,900 katika mji mdogo wa
Kisaki ambao ni lango la kuingilia Mradi wa Kufufua Umeme wa Stiglers
George na Hifadhi ya Taifa ya Mwl Nyerere zamani Selous.
Kwa
mujibu wa Mkuu huyo wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya wilaya ya
Morogoro, tayari maeneo tisa ya kufanyiwa urasimishaji makazi
yameanishwa aliyoyataja kuwa ni Pangawe, Mkambarani, Fulwe, Ngerengere,
Mvuha, Kisaki , Mtamba, Mkuyuni na Dhutumi na kubainisha kuwa
halmashauri yake imepokea na kuridhia maombi kutoka makampuni manne kwa
ajili ya kazi hiyo.
Wakati
huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi za Wakala wa
Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zilizopo katika wilaya ya Mvomero mkoani
Morogoro, ujenzi unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Akiwa
katika ukaguzi huo, Dkt Mabula mbali na kulipongeza Shirika la Nyumba
la Taifa kwa kuisimamia vyema miradi yake ya ujenzi katika maeneo
mbalimbali nchini ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa Ofisi hizo za TFS
hasa baada ya kuelezwa na Msimamizi wa ujenzi huo Mhandisi Grace Musita
kuwa hatua iliyofikiwa sasa na Shirika lake katika kujenga ofisi hizo za
TFS ilitakiwa kufikiwa tarehe 13 Desemba 2019.