JOSE MOURINHO AMRITHI MAURICIO POCHETTINO BAADA YA KUPIGWA KALAMU TOTTENHAM

Jose Mourinho na Mauricio Pochettino
Jose Mourinho ameteuliwa kuwa mkufunzi mpya wa Tottenham akichukua nafasi ya Mauricio Pochettino ambaye alifutwa kazi siku ya Jumanne.

Mourinho amepata kuwa mkufunzi wa Man United na Chelsea hapo kabla, na tayari ametia saini kandarasi ya kuinoa Spurs hadi mwisho wa msimu wa 2022-23. 

''Jose ni moja ya wa wakufunzi waliofanikiwa sana katika soka'', ameema mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy.

Pochettino mwenye umri wa miaka 47 alifutwa kazi kama mkufunzi wa Spurs Jumanne usiku baada ya kuhudumu katika klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Katika kipindi hicho, klabu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa London ilipata mafanikio ya kutajika na kuwa moja ya timu tishio England. 

Raia huyo wa Argentina aliiongoza Spurs kufika katika fainali ya kombe la klabu bingwa Ulaya msimu uliopita ambapo walipoteza kwa Liverpool.

Hata hivyo msimu huu umeanza vibaya, ambapo klab hiyo imekuwa ikipata vipigo vya mara kwa mara, ikiwemo kipigo cha 7-2 kutoka kwa Bayern Munich mwezi uliopita. 

Spurs kwa sasa ipo katika nafasi ya 14 ya msimamo wa ligi ya Primia wakiwa na alama 14, ikiwa ni alama tatu tu juu ya mstari wa timu zilizo hatarini kushuka daraja. 

Pia, kumekuwa na ripoti kuhusu mkwaruzano kati ya Pochettino na mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy.

Hali hiyo, imewalazimu wakuu wa Spurs kumpiga kalamu Pochettino na kusaka usaidizi wa mkongwe Mourinho. 

Mourinho ambaye ni raia wa Ureno amekuwa bila kazi ya ukufunzi tangu alipofutwa kazi na United mnamo Disemba 2018. 

Mkufunzi wa Bournemouth Eddie Howe, kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsmann na aliyekuwa kocha wa Juventus Masimilliano Allegri wote walikuwa wakihusishwa na uhamisho wa kujiunga na Spurs, lakini wamezidiwa kete na Mourinho.

Je, Spurs na Mourinho wataendana?

Spurs haijawahi kumsajili mkufunzi aliye na mahitaji ya kiwango cha juu zaidi kama Mourinho, na wala haijawahi kutumia fedha nyingi kuwanunua wachezaji kama vile alivyozoea katika klabu za Real Madrid na Man United. 

Hivyo basi mashabiki wengi watashangazwa kwamba huenda akajiunga na klabu hiyo huku kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsman akionekana kijana zaidi na mwenye uwezo wa kuongoza klabu hiyo.

Lakini Spurs katika miaka ya hivi karibuni wametoka mbali chini ya ukufunzi wa Pochettino . 

Wana uwanja mpya uliojengwa kwa thamani ya pauni bilioni moja na uwanja wa mazoezi mbali na kufuzu kushiriki katika ligi ya mabingwa mara nne mfululizo huku uuzaji wa baadhi ya wachezaji ukiwasaidia na kuifanya klabu kuwa klabu iliojipatia faida kubwa duniani. 

Kwa sasa wana kikosi chenye talanta.

Mourinho amekuwa nje ya ukufunzi kwa takriban mwaka mmoja sasa na huku akiendelea kuishi mjini London, kazi hiyo inamfaa sana.
chanzo BBC

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post