
Mkuu
wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro amewataka wazazi wote na
walezi Mkoani Mara walioozesha watoto wadogo wakiwemo wanafunzi
kurudisha ng’ombe walizopokea kama mahari vingenevyo watashughulikiwa
kwa mujibu wa sheria na watafungwa jela.
“Baba wa Tanzania hauko juu ya sheria ukimpiga mkeo ni kosa la jinai
ukimuozesha mwanao kabla ya umri ni kosa utashughulikiwa tu, lazima
tufunge watu sasa hata kama wazazi wamekubaliana tutawagonga kwa mujibu
wa sheria”amesema
Sirro ametoa agizo hilo Wilayani Bunda Mkoani mara wakati wa uzinduzi wa
madawati ya jinsia Mkoani humo ambapo akiwa Bunda ametoa agizo kwa
wazazi wote na walezi kuhakikisha wanawarudisha watoto wote
waliowaozesha na warudishe mahari kama wanataka mali wazitafute kwa
kufanyakazi na siyo kufanya watoto wa kike mtaji.
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi ameendeleza kauli mbiu yake ya polisi
kutumia nguvu ya kadri kwa wanaume wote nchini wanaopiga wake zao ili
kukomesha vitendo vya ukatili ambavyo amesema Mkoa wa Mara unaongoza kwa
ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
“Bahati mbaya sana mimi ni IGP na natokea Mkoa huu sasa kuanzia sasa huu
ukatili haukubaliki madawati haya ya jinsia yatafanyakazi saa ishirini
na nne mwana mama ukipigwa muda wowote wewe nenda kituoni utapata huduma
na huyo aliyekupiga atapata huduma anayostahili”ameongeza Sirro
Aidha amewaomba viongozi wa madhehebu ya dini wafanye kazi ya doria ya
kiroho kwa waumini wao ili waachane na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkuu wa wilaya ya Bunda Bi Lidya Bupilipili akimkaribisha IGP wilayani
hapa ameeleza kuwa mbali na ukatili kwa watoto lakini kuna changamoto ya
wanafunzi wa kike kutumia uzazi wa mpango wakati bado wanasoma.
Amesema wazazi wamewekeza kwenye mambo ambayo hayana tija badala ya
kuwekeza kwenye elimu ndiyo maana mmomonyoko wa maadili ni mkubwa.
“Sijawahi kushuhudia katika kesi nnazopokea ofisini kwangu baba amekatwa
mapanga lakini kila siku ni wanawake tu na jambo la kusikitisha kuna
baadhi ya viongozi wa vijiji hawalichukulii kwa uzito ukatili
huu”amesema mkuu wa wilaya
Mkurugenzi wa jukwaa la Utu wa Mtoto CDF bw Koshuma Mtengeti amewataka
wana Mara kuacha vitendo vya unyanyapaa kwa wahanga wa ukatili wa
kijinsia na wasiogope kwenda kutoa ushahidi wanapohitajika.
Ameongeza kuwa kamati za ulinzi na usalama zinapaswa kuhakikisha sheria zinasimamiwa kikamilifu kuanzia ngazi ya chini.