ELIMU YA KODI YAWAFIKIA WAFANYABIASHARA NA WANANCHI WA MALINYI

Afisa Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Julius Mjenga akiwaelimisha baadhi ya Wafanyabiashara wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.

Baadhi ya Wafanyabiashara wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakisikiliza elimu ya kodi kutoka kwa Afisa Kodi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Julius Mjenga (hayupo pichani) wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro wakijisomea kitabu cha Kodi na Ushuru Mbalimbali wakati wa Wiki ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa Mikoa ya Morogoro na Pwani.(PICHA ZOTE NA TRA)


Na Veronica Kazimoto-Malinyi
 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekutana na wafanyabiashara pamoja na wananchi wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ikiwa ni pamoja na kuwasajili wafanyabiashara wasiokuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi.

Akizungumza na wafanyabiashara hao wakati wa utoaji wa elimu hiyo, Afisa Kodi Mkuu wa TRA, Julius Mjenga, amewahimiza kutunza kumbukumbu za biashara zao ili kukadiriwa kodi stahiki.

“Mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kuwa TRA inawakadiria kodi kubwa lakini mlio wengi hamtunzi kumbukumbu kwenye daftari linaloonyesha manunuzi na mauzo ya kila siku ili mwisho wa mwaka Afisa wa Kodi atumie daftari hilo kukukadiria kodi ambayo inaendana na uhalisia wa biashara yako,” alisema Mjenga.

Mjenga ameongeza kuwa, mfanyabiashara anaetunza kumbukumbu analipa kodi kidogo ukilinganisha na mfanyabiashara ambaye hatunzi kabisa kumbukumbu za biashara yake.

Naye mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Samson Nyanda wa wilayani hapa, ameiomba TRA kutoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa kuwa wafanyabiashara huongezeka kila wakati.

“Elimu hii tuliyoipata ni nzuri mno ila tunaomba iwe endelevu na ifanyike hata kwa mwaka mara tatu kwa sababu kila wakati wafanyabiashara wanaongezeka na wengi wao hawana hii elimu ya utunzaji wa kumbukumbu”, alieleza Nyanda. 

Mamlaka ya Mapato Tanzania inafanya Kampeni ya Elimu, Usajili na Huduma kwa Mlipakodi katika Mikoa ya Morogoro na Pwani ambapo kwa Mkoa wa Morogoro, timu ya maafisa wa TRA inatarajia kuwafikia wafanyabiashara na wananchi wa Kilosa, Ulanga, Kilombero, Mvomero, Gairo na Morogoro vijijini.

Wakati katika Mkoa wa Pwani, timu ya maafisa wa TRA imelenga kuwafikia wafanyabiashara wote wa maeneo ya Kibaha, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga, Chalinze na Bagamoyo ambapo kampeni hiyo imeanza tarehe 11 na itamalizika tarehe 17 Novemba, 2019.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post