WAKENYA WAENDELEA KUFANYA VIZURI ROCK CITY MARATHON


Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Wanariadha kutoka nchini Kenya wameendelea kuwawanyanyasa wenzao kutoka mataifa jirani wakiwemo wenyeji Tanzania kwenye mbio za Rock City Marathon ambayo hufanyika jijini Mwanza yakiandaliwa na kampuni ya Capital Plus.
 
Kwa mwaka huu 2019 ikiwa ni mwaka wa10 tangu mbio hizo ziasisiwe zikiwa na malengo ya kutangaza utalii, kupinga mauaji kwa watu wenye ualibino pamoja na kuendeleza mchezo wa riadha, bado wakenya wameendelea kutesa kwenye mbio hizo zilizoanza na kumalizikia katika viunga vya Rock City Mall, Oktoba 20, 2019.
 
Wanariadha kutoka Kenya kila mwaka wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mbio ndefu za kilomita 21 na 42 ikilinganishwa
na nchi nyingine ikiwemo Uganda, Rwanda na wenyeji Tanzania.
 
Katika mbio za mwaka huu, mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21 upande wa wanaume ni Bernard Musau kutoka Kenya,
mshindi wa pili ni Ochieng Julius kutoka Uganda, mshindi wa tatu Alex Nizemana kutoka Rwanda, nafasi ya nne Willy Rono kutoka Kenya huku nafasi ya tano ikienda kwa mtanzania Chacha Boy.
 
Kwa wanawake mshindi wa kwanza hadi wa nne wote ni kutoka Kenya ambao ni Ester Kakuri, Vane Nyaboke, Ronah Nyabochoa
na Martha Njoroge huku mshindi wa tano akiwa ni Grace Jackson kutoka Tanzania.
 
Katika urefu wa kilomita 42 upande wa wanawake mshindi wa kwanza hadi wa tisa wote ni kutoka Kenya, walioshika nafasi
tatu bora ni Elilither Tanui, Joan Rotich na Lidia Wafula huku mtanzania Zainab Said akishika nafasi ya 10 ambapo kwa upande wa wanaume kwa nafasi ya 10 bora wakenya walikuwa tisa na mtanzania mmoja ambapo washindi wa nafasi ya kwanza
hadi ya tatu ni Abraham Too, Willium Koskei na John Muthui huku mtanzania Hamis Athuman akishinda nafasi ya nne.
 
Akizungumza katika mashindano hayo, mgeni rasmi Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla alisema mbio hizo
ni chachu ya kutangaza vivutio vya utalii katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza huku pia zikisaidia kukuza pato kwa Taifa na mtu mmoja mmoja.
 
Naye Mratibu wa mbio hizo, Magdalena Laiza aliwashukuru wadau wote waliosaidia kufanikisha mbio hizo ambazo zimekuwa
zikisaidia kuutangaza utalii wa ndani huku akisema mwakani mbio hizo zitakuwa bora zaidi na hivyo kuwahimiza washiriki wengi kujitokeza.
 
Mwanariadha Chacha Boy kutoka Tanzania alisema wanariadha wengi nchini hawafanyi vyema kwenye mashindano ya riadha
kutokana na kukosa maandalizi ya kutosha kwani wamekuwa wakijiandaa pale msimu wa mashindano unapowadia lakini baada ya mashindano ushirikiano baina yao, makocha pamoja na viongozi husambaratika.
 Mgeni rasmi, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangalla akizungumza kwenye kilele cha mbio hizo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post