WAITARA AOMBA WANANCHI KUCHAGUA VIONGOZI WENYE HOFU YA MUNGU

Image result for Naibu waziri waitara
 
 
Na Paschal Dotto-MAELEZO.
Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika nchi nzima Novemba 24, 2019, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mwita Waitara amewaomba viongozi wa Dini kuwahamsisha wananchi kuchagua viongozi wenye hofu ya Mungu.

Akizungumza katika Mkutano wa Kujadili namna Taasisi za Dini zinzvyochangia Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, Mhe. Waitara amesema kuwa ni muhimu kuwachagua viongozi wenye hofu ya Mungu na waadilifu kwa wananchi ili kuiunganisha Serikali katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
“Viongozi wa Dini nyie mnahubiri amani na haki, watu wakipata haki maana yake nchi inatulia, kwa hiyo hakikisheni mnawahubiria watu wenu kuhusu kuchagua viongozi walio na hofu ya Mungu ambao pia ni waadilifu kwa wananchi ili kuondoa migogoro mbalimbali ambayo imekuwa ikisababishwa na viongozi wala rushwa kwenye mitaa yetu ikiwemo ile ya ardhi”, ameeleza Mhe.Waitara.
Waziri Waitara alisema kuwa viongozi waadilifu huwa wanawajibika bila shida yeyote, kwa hiyo ni muhimu kuunganisha juhudi za Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa wananchi kwani uwajibikaji wake ni mkubwa katika kuwaletea maendeleo wananchi.
Alianisha sifa nzuri za kiongozi kuwa ni yule mwenye maono, maamuzi sahihi, anayesimamia maono na maamuzi yake, sifa ambazo Rais Magufuli anazo, kwa hiyo ili kuendelea kuleta maendeleo ni lazima viongozi wa Serikali za Mitaa ambako maendeleo yaanzia wawe waadilifu na wenye hofu ya mungu.
Waziri Waitara alisema kuwa mpaka Oktoba 17, 2019 wananchi milioni 19,686,000 walikuwa wamejiandikisha, sawa na asilimia 86 ikilinganishwa na mwaka 2014 ambapo wananchi Milioni 11 walijiandikisha sawa na asilimia 63.
Aidha Waitara alisema kuwa katika hatua za uchaguzi huo wagombea wataanza kuchukua fomu za kugombea kuanzia oktoba 29, 2019 na kwamba itakapofika Novemba 5, 2019 wasimamizi wa Uchaguzi watabadika majina ya wagombea kwa hiyo viongozi wa dini wanatakiwa kuwasaidia wananchi kujua kiongozi mwadilifu na pia kusali kwa ajili ya kupata kiongozi bora katika mitaa mbalimbali nchini.
Waziri Waitara alisema kuanzia Novemba 17 hadi 23, 2019, itakuwa ni muda wa kampeni ambapo amewataka wagombea kuomba kura kwa kujenga hoja kwa wananchi na kuwataka Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Dini kusimamia kikamilifu suala ya amani wakati wa kampeni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kuwa watu wanatakiwa kubadilika na kufuata kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wasaidizi wake kwani wanakimbizana kuwaletea maendeleo wananchi.
“Kuna watu bado hajabadilika na hawataki kubadilika, lakini ukiangalia makusudi ya Rais wetu, Makamu wake, Waziri Mkuu na Mawaziri wanakimbizana kuleta matokeo kwa wananchi, lakini huku chini ni shida kidogo, kwa hiyo nawaomba viongozi wetu wa Dini tuwahamasishe wananchi wetu Novemba 24, 2019 wajitokeze kuwachagua Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wenye hofu ya Mungu”, alieleza Makonda.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post