SERIKALI YAWATAKA MADIWANI KUTOA MAJINA YA MITAANaibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Vodacom, Michael Mjatta (wa kwanza kushoto) wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye kata ya Nyamtukuza wilayani Kakonko, Kigoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa diwani wa kata ya Nyabibuye, Stephine Mnigankiko wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye kata hiyo, Kakonko, Kigoma
Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Albert Richard akitoa taarifa ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyevaa koti) wakati wa ziara yake Kakonko, Kigoma ya kukagua huduma hizo
Mhandisi wa Vodacom, Michael Mjatta (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye (wa nne kulia) kuhusu upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi wa kata wa Nyamtukuza, Kakonko, Kigoma
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi wa Atashasta Nditiye (katikati) akimsikiliza diwani wa kata ya Nyamtukuza, Abdallah Magembe, wakati wa ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Kakonko, Kigoma. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Hosea Maloda
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, aliyesimama mbele katikati, akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wa Wilaya za Mkoa wa Kigoma baada ya kufungua mafunzo ya kujenga uelewa wa kufanikisha utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi yaliyofanyika, Kibondo

Na Prisca Ulomi, Kigoma

Serikali imewataka madiwani wote nchi nzima kutoa majina ya mitaa ili kufanikisha utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu umuhimu na manufaa ya kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi kwa madiwani, viongozi wa Serikali na watendaji mbali mbali wa Mkoa wa Kigoma yaliyofanyika wilayani Kibondo yaliyotolewa na wataalamu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania

“Madiwani tupeni majina ya mitaa ili vifurushi, barua na vipeto viwe vinakwenda moja kwa moja kwa wananchi, tufanye biashara mtandao na kuimarisha ulinzi na usalama,” amesema Nditiye.

Ameongeza kuwa biashara mtandao ni nzuri, tunataka kifurushi cha mtu kiletwe anapoishi na tayari nchi nzima kata zote zina postikodi, madiwani tupeni majina ya mitaa ili tuweke vibao na namba za nyumba ili wananchi watambulike

“Unaweza kupata postikodi ya kata au wadi yako kupitia simu yako ya mkononi kwa kupiga *152*00# kisha chagua 3 (ajira na utambuzi), 3 (TCRA – Postcode) endelea kufuata maelekezo hadi kupata postikodi ya kata yako”, amesema Nditiye.

Amefafanua kuwa utekelezaji wa mpango wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima unalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa na anwani yake ya mahali alipo iwe mahali pa kazi, nyumbani au ofisini ili kuwezesha mwananchi kuhudumiwa kwa urahisi. 

Ametoa rai kwa madiwani wote nchi nzima kutoa majina ya mitaa ili Wizara iweze kuweka nguzo zenye majina ya barabara na namba za nyumba au majengo katika maeneo yao kwa kuwa tayari kata zote nchi nzima zina postikodi.

Ameeleza kuwa kuna maneno yamezoeleka kuwa Dunia ni kama Kijiji, ili dunia iweze kuwa kijiji kunategemea uwepo wa mfumo wa utambuzi wa makazi na wakazi kwa ajili ya kurahisisha utoaji na ufikishaji wa huduma kwa wananchi ambapo anwani za makazi na postikodi zinawezesha utambuzi husika na nchi zilizoendelea zilishafika hatua hii na zinaendelea kunufaika na matunda ya utambuzi husika kijamii na kiuchumi 

Naye Mkuu wa Kanda ya Kati wa TCRA, Antonio Manyanda wakati akitoa mafunzo hayo amesema kuwa mpango wa anwani za makazi na postikodi utaongeza ajira kutokana na fursa za kusambaza bidhaa za wateja katika maeneo yao na mahali walipo; kurahisisha biashara mtandao hivyo kukuza uchumi; kuongeza mapato ya Serikali kwa kuwa mamlaka zinazohusika na ukusanyaji wa mapato zitakuwa na taarifa ya mahali walipo walipa kodi au wananchi hivyo kuwezesha ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi.

Manyanda amezitaja faida nyingine za mpango huo ni kurahisisha utoaji wa huduma mbali mbali za kijamii kama vile usajili wa mali, biashara, vizazi na vifo; kuongeza usalama kwa wananchi kwa kutoa huduma za dharura kwa wakati kwa mfano matukio ya moto,ugonjwa na uhalifu; kuboresha utendaji wa taasisi mbali mbali kwa mfano benki kuwa na uhakika wa mahali anapopatikana mteja wakati wa utoaji na urejeshaji wa mkopo; kurahisisha utambulisho wa watu na mahali wanapoishi; na kuwezesha utambuzi na mwelekeo na eneo ambalo mtu anahitaji kwenda 

Wakati akimkaribisha Nditiye, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibondo, Ayubu Sebabili amesema kuwa wako tayari kutekeleza mpango huo ili wananchi waweze kuuza na kununua bidhaa kutoka ndani nan je ya nchi na kupelekea sehemu nyingine duniani kwa urahisi na wakati hivyo kuongeza ajira na kipato kwa wananchi

Katika hatua nyingine, Nditiye amekagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano wilayani Kibondo kwa kutembelea minara iliyopo kata ya Nyabibuye na Nyamtukuza iliyojengwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambapo alielekeza kampuni za simu za mkononi kuongeza nguvu ya minara hiyo ili iweze kutoa huduma ya data badala ya sauti pekee kutoka teknolojia ya 2G hadi kufikia teknolojia ya 3G 

“Maeneo mengi watu walianza na 2G, tunao waalimu, madaktari, siku hizi kuna wasomi wengi sana vijijini, nimewaelekeza UCSAF washirikiane na kampuni za simu ili kuhakikisha kuwa minara iliyopo vijijini inatoa huduma za 3G ili huduma hii itupe fedha Serikalini kwa kuwa ukitumia data unalipa gharama,” amesema Nditiye
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Maloda Ndagala amemweleza Nditiye kuwa intaneti ni ndogo hata mtu akikutumia nyaraka kwa what’s app inachukua muda mrefu kufunguka
Akiwa ziarani Wilayani Kakonko, Nditiye ametoa rai kwa viongozi wa Wilaya hiyo kuelimisha wananchi umuhimu wa kusajili laini za simu kwa alama za vidole na kutekeleza mpango wa anwani za makazi na postikodi

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post