WAKANDARASI MRADI WA MAJI SAME-MWANGA WATAKIWA KUONGEZA KASI

Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa maji wa Same-Mwanga wametakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili ukamilike kwa wakati.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa maelekezo hayo Septemba 28, 2019 wakati wa ziara yake iliyolenga kukagua hatua ya ujenzi iliyofikiwa na Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo ambao ni kampuni ya M.A Kharafi & Sons na kampuni ya Badr East Africa Enterprises.

Mara baada ya kujionea shughuli zilizokuwa zikiendelea na kupokea taarifa ya mradi kutoka kwa wakandarasi hao, Mhandisi Sanga alieleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezwaji wake na aliwasisitiza kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa wakati.

Mhandisi Sanga aliwataka Wakandarasi kuwa wepesi kwenye kufanya mawasiliano na Wizara kila wanapokutana na changamoto yoyote ambayo ipo nje ya uwezo wao ili ufumbuzi upatikane haraka bila kuchelewesha shughuli za ujenzi wa mradi.

“Sijaridhishwa na kasi yenu ya ujenzi wa mradi. Kama kuna changamoto mnakutana nazo zilizo nje ya uwezo wenu mhakikishe mnawasiliana na Wizara mapema iwezekanavyo ili tupate ufumbuzi,” alisema Mhandisi Sanga.

Aliongeza kwamba Serikali inachohitaji ni kuona matokeo na haipo tayari kumvumilia mkandarasi ambaye anachelewesha mradi bila ya kuwa na sababu za msingi.

“Wanachohitaji wananchi ni maji, Serikali haitomvumilia Mkandarasi ambaye atashindwa kwenda na kasi inayokubalika,” alibainisha Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga vilevile aliwakumbusha wakandarasi hao kuhakikisha manunuzi ya vifaa vinavyohitajika kwenye ujenzi wa mradi huo yanafanyika hapa nchini badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba vingi vinapatikana hapa hapa Nchini.

Wakandarasi hao kwa nyakati tofauti walimuahidi Naibu Katibu Mkuu Sanga kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi sambamba na kuzingatia maelekezo aliyoyatoa.

Mradi wa Same-Mwanga ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuondoa kero ya maji kwa wakazi wa Miji ya Same na Mwanga, Mkoani Kilimanjaro na baadaye Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga.

Ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu Sanga kwenye mradi huo ni ya kwanza tangu ameteuliwa na kuapishwa kushika wadhifa huo Septemba 22, 2019

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post