SIMANJIRO YA KIJANI YAMKUNA POLEPOLE, AMFAGILIA OLE MILYAKatibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole akizungumza kwenye kongamano la Simanjiro ya kijani lililofanyika Mji mdogo wa Mirerani na kuandaliwa na UVCCM Simanjiro.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza kwenye kongamano la Simanjiro ya kijani lililofanyika Mji mdogo wa Mirerani.

KATIBU wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole amemfagilia Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara James Ole Millya (CCM) kuwa ni mchapakazi na anayewajibika kwa wananchi.

Hata hivyo, Polepole amewashukia vikali baadhi ya wanachama na makada wa CCM wanaoiwania nafasi hiyo ili hali mbunge wa jimbo hilo Ole Millya (CCM) anaendelea na nafasi hiyo.

Polepole ameyasema hayo kwenye kongamano la Simanjiro ya kijani lililofanyika Kata ya Endiamtu Mji mdogo wa Mirerani na kuandaliwa na Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Simanjiro.

Amesema Ole Millya ni kijana mwenye nguvu hivyo viongozi wa CCM na wa serikali wa wilaya ya Simanjiro wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha ili wawatumikie wananchi.

“Tumekubaliana kwenye vikao vikubwa vya chama kuwa mahali palipo na mbunge wa CCM hapaswi kubuguziwa wala kuguswa na mtu yeyote wala hata wale wa CCM waache unyemelezi,” alisema Polepole.

Pia, amewakemea vikali baadhi ya viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wenye siasa chafu ambao wanataka kumkwamisha Ole Millya katika nafasi hiyo.

“Hivi sasa tuna mbunge mmoja jimbo la Simanjiro naye ni Ole Millya, anapaswa kuachiwa nafasi hiyo kwani atatekeleza ilani ya CCM kwenye eneo hilo hivyo apewe nafasi afanye kazi yake,” alisema Polepole.

Amemtaka Ole Millya afanye kazi yake kwa uadilifu kwa kuwatumikia bila wasiwasi wowote wananchi wa Simanjiro ambao wana kiu kubwa ya maendeleo.

Alisema Ole Millya ni kiongozi mzuri anayefanya kazi amekuwa akimshirikisha kwenye baadhi ya changamoto za wilaya hiyo ikiwemo migogoro ya ardhi hadi anajiuliza kwa nini hawana umoja.

“Wengine huwa wanaogopa kupigwa mzinga, sasa wewe tumekuchagua unataka mzinga apigwe nani, hiyo ndiyo kazi yako ukipigwa mzinga toa, wananchi wako wakikudipu (beep) wapigie kwani hiyo ndiyo kazi yako kwao unaowaongoza,” alisema Polepole.

Kwa upande wake, James Ole Millya alimuomba Polepole akemee makundi na mgawanyiko unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM wa wilaya hiyo wanaokata majina ya wagombea.

“Simanjiro kuna tatizo kubwa la baadhi ya viongozi kukata majina ya wagombea kwa sababu hawaungi mkono au kuwa kwenye kambi yao,” alisema Ole Millya.

Alisema yeye anafanya kazi kwa moyo mmoja wa kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wala matabaka ila hafurahishwi na tabia ya baadhi ya viongozi wa CCM kukata majina ya wagombea.

Alisema hakuna sababu ya kukata majina ya wagombea wa CCM hasa kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa ili mradi siyo jambazi au hana sifa mbaya.

Mmoja kati ya wakazi wa wilaya hiyo, Meshak Laizer alisema maendeleo yaliyopatikana Simanjiro kwa kipindi cha miaka minne ya ubunge wa Ole Millya ni makubwa sawa na miaka 20.

“Tunaona lami Mirerani, vituo vya afya vimeboreshwa, hospitali ya wilaya, jengo la utawala la halmashauri na maji ya mto Ruvu hadi Orkesumet tunamshukuru Rais John Magufuli kwa kutupatia fedha za maendeleo,” alisema.

Alisema pia mbunge huyo ni kiunganishi cha wananchi kwani tangu akiwa mbunge kwa tiketi ya Chadema hakubagua na sasa yupo CCM hana makundi wala kambi.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post