SHIVYAWATA Waiomba Serikali kutilia Mkazo Ukatili wa Kijinsia kwa Watu wenye Ulemvu

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma Magwiza (Kushoto) akielezea namna Wizara inavyoshugulikia masuala ya ukatili dhidi ya watoto wakiwemo wenye ulemavu katika kikao kati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo kinachoshughulikia watu wenye ulemavu.
SHIRIKISHO la Vyama vya Walemavu (SHIVYAWATA) limeiomba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia, Wazee na Watoto kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma juu ya kupambana na manyanyaso na vitendo ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu nchini.

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Taifa Ummy Hamisi Nderiananga wakati wa kikao kati ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo kinachoshughulikia watu wenye ulemavu.

Ummy ameongeza kuwa kama Wizara ilivyoweka nguvu kwenye masuala ya jinsia hasa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto basi pia waongeze nguvu katika kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya walemavu katika jamii.

“Vitendo vya ukatili dhidi ya walemavu wawe watoto au wanawake hata wanaume pia vinatendeka katika familia zatu ila havipigiwi kelele za kutosha” alisema Ummy.

Ummy amesisitiza Wizara kupitia Mpango Mkakati wa Taifa wa kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ili uweze kuwezesha kuingiza masuala ya watu wenye ulemavu ili kuondokana na vitendo vya kikatili vinavyowapata watu wenye ulemavu nchini.

Akifafanua kuhusu Wizara kutilia Mkazo suala la Ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwajuma Magwiza amesema kuwa Wizara inalenga kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya makundi yote ikiwemo kundi la watu wenye ulemavu nchini.

Mwajuma ameongeza kuwa Wizara imejikita katika Kampeni mbalimbali za kupambana na vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto likiwemo kundi la watu wenye elemavu kwa kutoa elimu kwa jamii ya kupambana na vitendo hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amesema kuwa kikao hicho kimeisaidia Wizara kupata namna bora ya kuyafikia makundi ya watu wenye ulemavu kabla ya kuandaa miongozi na Mikakati mbalimbali ya Wizara ili katika utekelezaji wake isiache kundi la watu wenye ulemavu na makundi mengine maalum.

Golwike ameongeza kuwa Wizara itashirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha watu wenye ulemavu katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu katika kapata fursa sawa kama makundi mengine katika jamii hasa katika utoaji wa mikopo na elimu ya ujasirimali.

Naye Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Philbert Kawemama amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inafuatilia utekelezaji wa Sheria namba 9 ya mwaka 2010 na Kanuni zake ili kuhakikisha kila Wizara na Taasisi zake zinazingatia masuala ya watu wenye ulemavu katika kuhakikisha wanapata mazingira stahiki katika utekelezaji wa majukumu yao.

Ameongeza kuwa pia Ofisi ya Waziri Mkuu inafuatilia uwezeshwaji wa kundi la watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa za kimaendeleo na kusaidia kundi hilo kuondokana na vitendo vya unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi yao.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la ADD International Isack Idama amesema kuwa Wizara ina dhamana kubwa kwa maendeleo ya watoto na wao kama wadau wa masuala ya watu wenye ulemavu hasa watoto wangependa kuona kwa jinsi gani masuala ya watoto wenye ulemavu yanashughulikiwa.

Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo kinachoshughulikia watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania wanatembela Wizara na Taasisi za Serikali katika kufuatilia na kuona kwa jinsi gani masuala ya watu wenye ulemavu yatekelezwa.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post