RAIS MAGUFULI: SABABU YA NDEGE YA TANZANIA KUKAMATWA AFRIKA KUSINI NI WIVU


Rais Dkt John Pombe Magufuli amesema kuwa sababu ya ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kukamatwa nchini Afrika Kusini ni wivu, kutokana na shirika hilo kuanza kuimarika na kuteka masoko mbalimbli ndani na nje ya Afrika.

Rais ameyasema hayo leo asubuhi alipokuwa akizindua kituo cha mfumo wa rada ya kuongozea ndege katika kituo cha Dar es Salaam, ambayo ni moja ya rada mpya nne zitakazofungwa nchini na kuwezesha kuona na kuongoza ndege katika anga lote la Tanzania.

“Ukiona hadi watu wanakamata ndege zetu basi ujue shirika letu linafanya kazi vizuri,” alisema Rais Magufuli

Amesema kuwa licha ya kukamatwa kwa ndege hiyo (ambayo tayari imeshaachiliwa) ataendelea kuchapaka kazi, huku akitolea mfano kutoka kwenye mashairi ya wimbo wa kundi la Sauti Sol la Kenya, wimbo unaoitwa Extravaganza ambao mashairi hayo yanasema, wakifunika, tunafua, wakianika, tunaanua, wakitufungia milango, wanatukuta ndani.

Rais ametoa pongezi kwa ATCL kwa namna ambavyo limekuwa likikua huku akieleza kwamba wakati lilipoanza safari zake lilikuwa likimiliki asilimia tatu pekee ya soko la ndani, lakini sasa linamiliki asilimia 75. Ameongeza kuwa, tayari shirika hilo limeanza safari za kimataifa, na karibuni litaanza kwenda China, hivyo ni lazima washindani wake waone wivu.

Akizungumzia rada iliyopaswa kununua kipindi cha nyuma, Rais ameonesha kukerwa kwamba fedha za Watanzania zilitafunwa na watu wachache na rada hiyo iliyokuwa inunuliwe nchini Uingereza haikusimikwa tena, hivyo mabilioni ya fedha yakawa yamepotea. Amesema aliwashangaa waliohusika kwenye sakata hilo kutokujiuzulu, angali wale wa upande wa Uingereza walijiuzulu.

Baada ya mifumo mipya ya rada za kuongozea ndege kukamilika kusimikwa, Tanzania itaweza kuona na kuongoza angala lote la nchi, tofauti na awali ambapo ilikuwa inaweza kuongoza asilimia 25 pekee ya anga lote.

Kuwa na uwezo wa kuongoza anga lote kutaongeza mapato ya serikali, kutaongeza kasi ya ndege kuweza kuruka na kutua katika viwanja vya Tanzania, hatua itakayoongeza abiria, lakini pia hatua hiyo ni kukidhi vigezo vya kimataifa.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post