MAMIA YA WAOMBOLEZAJI WAJITOKEZA KUMZIKA MTOTO WA MKUU WA MAJESHI ALIYEFARIKI KWA AJALI YA NDEGE

Na Stella Kalinga, Simiyu RS

Mamia ya wananchi kutoka mikoa ya Simiyu, Mara, Shinyanga, Mwanza na Dar es Salaam wameshiriki katika mazishi ya mtoto wa Mkuu wa Majeshi  marehemu Nelson Mabeyo aliyekuwa rubani wa ndege ya Shirika la Auric Air, ambaye alifariki Septemba 23, 2019 kwa ajali ya ndege iliyotokea katika Uwanja mdogo wa Seronera  uliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.


Mazishi hayo yamefanyika Septemba 26, 2019 katika Kijiji cha Masanzakona wilaya ya Busega Mkoani Simiyu, ambapo yalitanguliwa na ibada ya mazishi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Yuda Tadei lililipo kijijini hapo ambapo ni nyumbani kwao na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo.

Akihubiri wakati wa ibada ya mazishi, Askofu Michael Msonganzila, Jimbo Katoliki Musoma amewasihi waombolezaji wote kuendelea kuifariji na kuiombea familia ya Mkuu wa Majeshi ili wapokee msiba huo kwa jicho la imani, masikio ya imani na kama mpango wa Mungu.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akitoa salamu za serikali  amesema “marehemu Nelson Mabeyo alikuwa  kijana mcheshi na mchapakazi leo hatuko naye tena nitoe pole kwa familia ya Jenerali Mabeyo, sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea niwaombe tuendelee kuwaombea katika kipindi hiki kigumu Mwenyezi Mungu awape ustahimilivu.”

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka akizungumza  kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Simiyu na wakuu wa mikoa ametoa pole kwa familia ya Mkuu wa Majeshi na kumshukuru kwa namna Mkuu  alivyowaunganisha watu wa Masanza, Busega na Simiyu katika masuala mbalimbali ya  ikiwemo Ujenzi wa Kanisa ambalo ibada ya mazishi ya marehemu Nelson imefanyika.

Kwa upande wake  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenrali Venance Mabeyo amewashukuru watu wote walioshirikiana na familia yake tangu msiba wa mwanaye Nelson ulipotokea , ambapo amesema kama familia hawauchukulii msiba huo kama adhabu bali makusudi ya Mungu mwenyewe kwa mtoto wao .

Mazishi ya marehemu  Nelson Mabeyo yalihudhuriwa na  watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, viongozi na Maafisa wa JWTZ walioko kazini na wastaafu, mawaziri na manaibu waziri, makatibu wakuu, wakuu wa Taasisi, viongozi wa Vyombo vya Usalama, wabunge, Wakuu wa mikoa ya Simiyu, Mara, Shinyanga, Kagera, Kigoma, Mwanza na Dar es salaam , kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Simiyu na wakuu wa wilaya.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post