MAKALA - Serikali kuongeza bajeti utafiti wanyapori

  • Tanapa, Tawiri kushiriki utafiti wanyamapori waliotoweka

  •   Yafanikiwa kurejesha Mbwa mwitu hifadhi ya Serengeti


Seif Mangwangi

MBWA Mwitu ni miongoni mwa wanyamapori ambao wanaelezwa kuwa katika hatari kubwa ya kutoweka duniani kufuatia kuuawa kwa wingi pamoja na kukumbwa na magonjwa hatari. Hivi sasa wanyama hawa wanapatikana katika nchi saba pekee duniani ambazo ni Tanzania, Kenya, Botswana, Zimbabwe, Zambia, Afrika Kusini na Lesotho.

Tishio la kutoweka kwa wanyama hao nchini lilijitokeza mwaka 1994 baada ya kundi la mwisho kuondoka katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kukimbilia kwenye makazi ya watu jirani na hifadhi hiyo.

Mbwa mwitu ambao nchini pia hupatikana katika hifadhi za Ruaha na pori la Akiba la Selous na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, wanaelezwa kukimbia ndani ya hifadhi ya Serengeti baada ya wengi wao kufa kufuatia kukumbwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa pamoja na Kichaa cha Simba ‘Canaid Center virus. Hata hivyo huko walipokimbilia pia huuawa kwa wingi kufuatia kula mifugo ya wanavijiji.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prf Jumanne Maghembe akikata utepe kuashiria
kuachiliwa kwa mbwa mwitu kundi la sita ndani ya hifadhi ya Serengeti, watatu kulia kwake ni Balozi wa
Ujerumani nchini Egon Karionke na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa TANAPA Allan Kijazi. (PICHA NA
SEIF MANGWANGI)Hata hivyo Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa kushirikiana na mashirika mengine ikiwemo taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI), waliamua kushirikiana kutafiti sababu ambazo zimepelekea kutoweka kwa wanyama hao.

Kwa mujibu wa Mtafiti Mwandamizi katika taasisi ya utafiti wanyamapori Tawiri, Dkt Eblate Mjingo, baada ya kutoweka kwa wanyama hao, mwaka 2005 waliamua kufanya utafiti na hatimaye waliweza kugundua kuwa Mbwa Mwitu hao walitoweka baada ya kukumbwa na magonjwa ya kichaa cha mbwa na kichaa cha simba.

“Mbwa mwitu ni mnyama muhimu sana katika hifadhi hasa Serengeti yenye wanyama wengi, ambao wamekuwa na kazi moja tu ya kupunguza idadi ya wanyama kwa kuwa wao ni wanyama wanaokula nyama,”anasema.

Anasema baada ya kugundua tatizo lililopelekea kutoweka kwao ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti, timu ya watafiti ikaamua kujenga eneo maalum la kuwahifadhia wanyama hao na kuanza kuwakamata kutoka katika maeneo ya jirani na kuwaweka katika eneo hilo kabla ya kuwaachia na kutawanyikia porini.

 “Kundi la kwanza tulianza kulitoa mwaka 2012 baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, tunachokifanya hivi sasa ni kuwavalisha mikanda inayoendeshwa kwa kutumia satellite hivyo tunakuwa tunajua kila baada ya saa moja wanakuwa wapi,”anasema.

Anasema mikanda hiyo yenye uwezo wa kusoma GPS, hutumika kutambulisha wanyama hao maeneo wanayopendelea kutembea na endapo watatoka nje ya hifadhi watajulikana wameelekea wapi na hivyo kuwatafuta na kuwarejesha hifadhini.

Akizungumza katika hafla ya kufungulia kundi la sita la Mbwa Mwitu hao, katika eneo la Nyansori ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti,  aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Professa Jumanne Maghembe amesema idadi yao imeongezeka na kufikia 120.

Mtafiti Mkuu Mwandamizi wa taasisi ya utafiti wanyamapori (TAWIRI), Dkt Eblate Mjingo
akizungumza na mwandishi wa makala hii, Seif Mangwangi kuhusu utafiti wa Mbwa mwitu unaofanyika
ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti. (PICHA NA SEIF MANGWANGI)


Kundi hilo lenye idadi ya mbwa mwitu 17 imelezwa kuwa wamekaa katika eneo hilo la hifadhi kwa takribani miezi sita kwa lengo la kuwazoesha mazingira ya Serengeti kabla ya kuachiwa.

Hata hivyo Maghembe anasema Serikali itaongeza bajeti ya utafiti wa wanyamapori ikiwemo utafiti wa Mbwa Mwitu ili kurejesha mfumo wa ekolojia wa wanyama hao ulioanza kupotea na kusababisha kutoweka kwa baadhi ya makundi ya wanyamapori nchini.

Anasema bila utafiti wa wanyamapori na kugundua changamoto zinazowakabili sehemu kubwa ya wanyama hao wataendelea kutoweka na kubakia kuwa historia huku Serikali ikipoteza fedha nyingi za kigeni zinatotokaa na uwepo wa wanyama hao.

“Tunaendelea kukusanya fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi na katika bajeti ijayo tutaongeza fedha kwaajili ya wanasayansi katika utafiti wa wanyamapori ili kurejesha vizuri mfumo wa ekolojia wa wanyama hao ikiwemo mbwa mwitu na kuwaokoa katika hatari ya kutoweka, pia tutaongeza idadi ya watafiti na vifaa vya kutosha,”anasema.

Professa Maghembe anasema kiasili kila mnyama ameumbwa kwa malengo fulani na ndio maana kuna wanyama wanaokula majani na wanyama wanaokula nyama na hivyo kuwafanya kila mmoja kuwa na faida yake.

“Kila mnyama ndani ya hifadhi amekuwa na faida yake, hawa mbwa mwitu wamekuwa na faida kubwa katika mfumo wa ekolojia ambapo kazi yao kubwa ni kula wanyama wenzao ikiwemo waliozeeka, endapo hawatafanya hivyo wanyama wataongezeka na kumaliza malisho yaliyokuwepo,”anasema.

Professa Maghembe anasema Wizara ya Maliasili na utalii sio ya kuipuuza kwa kuwa imekuwa ikiingizia Serikali pato kubwa linalofikia asilimia 17 na kwamba ukijumuisha na misitu inafikia asilimia 20 kwa mwaka.

Meneja mradi huo wa utafiti wa Mbwa Mwitu kutoka taasisi ya Tawiri, Emanel Masenga anasema Mbwa mwitu katika hifadhi ya Serengeti wamekuwa wakitunzwa na kulishwa mbuzi ambao hununuliwa kutoka kwa wafugaji waliokuwa jirani na hifadhi ya Serengeti.

Anasema mbuzi ambaye hulishwa Mbwa mwitu hao, huchunwa ngozi ili kuondoa harufu itakayotambulisha aina ya mnyama anayeliwa na hivyo kumuepusha na mazoea kuwa anakula mbuzi jambo ambalo linaweza kusababisha wakakimbilia vijijini na kuanza kushambulia mbuzi. Kwa siku mbwa mmoja hula kilo nne za nyama na kukaa siku moja kabla ya kula tena.

Masenga anasema wamekuwa wakiwakamata mbwa mwitu hao kutoka katika maeneo ya jirani kwa kuwapiga sindano za usingizi kisha kuwapakia katika magari na kuwafikisha ndani ya eneo lililotengwa kwaajili ya kuwatunza.

“Kwa kawaida tunamuacha mnyama aishi maisha ya kiasili lakini kwa hawa tumelazimika kuwarejesha sababu wanatoweka, sehemu ya Makundi ya Mbwa Mwitu yamekimbilia vijijini, tunachofanya ni kuwakamata kutoka katika maeneo hayo na kuwahifadhi kwa miezi sita katika eneo maalum lililozungushiwa uzio kuzuia wasitoroke kabla ya kuwaachilia,”anasema na kuongeza:

“Hivi sasa tuna idadi ya mbwa mwitu 120 ndani ya hifadhi ya Serengeti, kupitia makundi sita yaliyokuwa yameshahifadhiwa hapa ndani  hii ni faraja sana kwetu kwa kuwa baadhi ya watalii hupenda kuangalia tu wanyama hawa, sasa wakikosekana ni hasara kwa Taifa kwa kuwa tunakuwa hatujamfurahisha mtalii,”anasema.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi anasema utafiti huo wa mbwa mwitu unaofanywa na taasisi ya utafiti wa wanyamapori nchini (TAWIRI), utasaidia kuepusha migogoro na wananchi kufuatia makundi ya mbwa mwitu kutorokea katika eneo la Loliondo na kuanza kula mbuzi na kondoo.

Anasema pia kuachiliwa kwa Mbwa mwitu hao na kuwarejesha katika maeneo yao ya  asili ni msaada mkubwa kwa Serikali kwa kuwa watasaidia kurejesha mfumo wa ekolojia na kuongeza utajiri wa wanyamapori ndani ya hifadhi ya Serengeti.

Mtafiti Mkuu Mwandamizi kutoka taasisi ya Tawiri Dkt Eblate Mjingo anasema hivi sasa kuna Mbwa mwitu mmoja miongoni mwa kundi hilo la sita amezaa hivyo wanaendelea kumuhudumia katika kituo hicho kabla ya kumuachilia.

Maisha ya Mbwa mwitu

Mtafiti Eblate Mjingo anasema kwa kawaida Mbwa mwitu ambao huishi katika makundi huweza kubeba mimba mara mbili kwa mwaka na mimba hiyo hukaa kwa siku 70 kabla ya kujifungua. Pia huzaa kati ya watoto 12 hadi 18 kwa mara moja. Hata hivyo katika kila kundi Mbwa mwitu mmoja pekee ndio hubeba mimba.

Kundi la Mbwa Mwitu waliokuwa wamehifadhiwa katika eneo maalum ndani ya hifadhi ya
Taifa ya Serengeti wakikimbia kuingia porini ndani ya hifadhi hiyo baada ya kuachiliwa. ( PICHA NA SEIF
MANGWANGI).


Anasema maisha ya Mbwa mwitu hutegemeana na eneo analoishi ambapo endapo akiishi maisha ya kiasili huishi miaka 6 hadi 7 lakini akiishi maeneo yaliyotengwa na kufuatiliwa (zoo), huishi hadi kufikia miaka 10 tangu kuzaliwa.

Mjingo anasema Mbwa mwitu ambao kiasili ni mnyama mpole kwa binaadam wamekuwa wakivutia katika uwindaji ambapo humkimbiza mnyama na kuanza kumla kwa kumdonoa huku akiwa anaendelea kukimbia au kasimama.

“Mbwa mwitu humla mnyama akiwa katika harakati za kukimbia, hufanya hivyo kwa sababu hawana uwezo wa kumuangusha mnyama hivyo hugawanyika makundi matatu, kundi la kwanza husimama kulia kwa mnyama na la pili kushoto kwake wakiendelea kumla huku kundi la mwisho likifanya ulinzi kuhakikisha wanamtisha mnyama asikimbie,”anasema.

Hata hivyo utafiti wa Mbwa mwitu unaelezwa kuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa fedha za utafiti, vifaa kama magari na kwamba hali hiyo imekuwa ikisababishwa na namna ambavyo jamii imekuwa ikipokea mradi huo kufuatia kufanywa na watanzania wenyewe. Utafiti huo hugharimu Milioni 150 kwa mwaka.

seifmangwangi@gmail.comThis is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post