Na, Egidia Vedasto, APC Media, Arusha.
Watetezi wa haki za wanawake na mitandao inayopinga ukatili wa kijinsia mkoani Arusha wamelaani vikali matukio ya mauaji yanayoendelea kujitokeza mkoani humo na maeneo mengine nchini, huku wakivitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali wote wanaobainika kuhusika na vitendo hivyo ili kukomesha hali hiyo.
Watetezi hao wameyasema hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, ambapo pia wamevipongeza vyombo vya habari mkoani humo kwa juhudi zao za kuibua na kuripoti matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia yanayotokea katika jamii.
Mtetezi wa mtandao wa kupinga ukatili wa kijinsia, Flora Mpesha, amewataka wanawake kujenga utamaduni wa kusikilizana na kuwaheshimu wenza wao ili kupunguza migogoro ya kifamilia inayoweza kuchochea vitendo vya ukatili.
Amesema wanawake wanapaswa kujenga mazungumzo yenye kuheshimiana katika familia, akieleza kuwa kusikilizana kati ya wanandoa kunaweza kusaidia kupunguza migogoro na kuzuia matukio ya ukatili.
Ameongeza kuwa baadhi ya wanaume hukosa maeneo salama ya kueleza hisia na changamoto zao, hali inayoweza kuwafanya kujikusanyia hasira na hatimaye kushindwa kujizuia wanapokumbwa na migogoro.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CAIC Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa Dunia Salama Foundation, Idd Ninga, amekemea na kulaani matukio ya ukatili na mauaji yanayoendelea mkoani Arusha, huku akiiomba Serikali kupitia vyombo vya dola kuwakamata na kuwachukulia hatua kali wote wanaohusika.
Ninga amependekeza kuundwa kwa kikosi maalumu cha Jeshi la Polisi kitakachokuwa na jukumu la kufuatilia na kuchunguza matukio yote ya mauaji ya wanawake, pamoja na kuanzishwa kwa kampeni maalumu za kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia.
Aidha, amevitaka vyombo vya habari kuendelea kutumia nafasi yao kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ukatili, kuibua matukio yanayotokea na kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kukabiliana na tatizo hilo.
Naye Mwanamtandao wa Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Jamii za Pembezoni, Ruth Allan, amesema migogoro ya kifamilia haipaswi kuwa sababu ya kupoteza maisha ya mwanamke au mwanaume, akisisitiza umuhimu wa kutafuta suluhu za amani wakati wa kutatua changamoto za kifamilia.
Amesema licha ya kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya mauaji mkoani Arusha, hajaona hatua kali zinazochukuliwa na vyombo vya dola dhidi ya wahusika, hali inayotia wasiwasi kuhusu usalama wa wanawake katika jamii.
Ruth ameongeza kuwa mauaji ya wanawake yanasababisha ongezeko la watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, wakiwemo watoto wa mitaani, kutokana na kupoteza wazazi wao.
Hata hivyo, amewataka wanawake kujiondoa katika mahusiano wanayobaini kuwa na viashiria vya ukatili ili kujikinga na migogoro inayoweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha, huku akivipongeza vyombo vya habari mkoani Arusha kwa juhudi zao za kuibua na kuripoti matukio ya ukatili, akisema vinastahili pongezi kubwa kwa mchango wao katika kuelimisha jamii.

