IPU YATAKA MABUNGE KUCHUKUA HATUA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

Na Seif Mangwangi, Arusha

RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amezitaka mamlaka za mabunge duniani kuimarisha sheria, uwekezaji na usimamizi wa huduma za afya ili kuhakikisha vifo vya wanawake, watoto wachanga na watoto vinavyoweza kuzuilika vinamalizika.

Dkt. Tulia ametoa wito huo Leo Oktoba 8,2026 wakati akifungua mjadala wa pamoja wa kibunge kuhusu afya ya wanawake, watoto wachanga, watoto na vijana, unaoendelea pembezoni mwa Mkutano wa 153 wa IPU unaoendelea Jijini Arusha, Tanzania.


Amesema afya ya wanawake, watoto wachanga, watoto na vijana si suala la maendeleo pekee, bali ni haki ya msingi inayohitaji dhamira ya kisiasa, uwekezaji endelevu na uwajibikaji kutoka kwa serikali na mabunge.

Kwa mujibu wa Dkt. Tulia, mabunge yana nafasi kubwa katika kuhakikisha kunakuwa na sheria zinazolinda afya na haki za wanawake, watoto na vijana, sambamba na kusimamia utekelezaji wa sera na mipango ya afya kwa manufaa ya wananchi.

Amesema hatua ya kwanza ni kuimarisha sheria zinazolinda haki za makundi hayo, huku hatua ya pili ikiwa ni kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya msingi, afya ya mama na mtoto mchanga, afya ya watoto na vijana, lishe pamoja na afya ya uzazi.

Dkt. Tulia pia ameyataka mabunge kuimarisha usimamizi na uwajibikaji kwa kuhoji iwapo fedha na rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya afya zinawafikia wananchi na kama sera zinazopitishwa zina matokeo yanayopimika.


Amesema matumizi ya takwimu na ushahidi wa kisayansi ni muhimu katika kubaini maeneo yenye changamoto na kupunguza tofauti za upatikanaji wa huduma za afya, huku akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wanawake, vijana na jamii katika maamuzi yanayohusu afya na maisha yao.

“Wajibu wetu lazima uwe wazi, kutoka kwenye dhamira hadi utekelezaji, kutoka utekelezaji hadi uwajibikaji na kutoka uwajibikaji hadi matokeo,” amesema Dkt. Tulia katika kusisitiza umuhimu wa hatua za vitendo.

Aidha, amesema IPU itaendelea kushirikiana na wabunge na wadau wa afya duniani kujenga uwezo wa mabunge kutunga sheria zenye ufanisi, kusimamia utekelezaji wa sera za afya na kudai uwajibikaji katika utoaji wa huduma.

Dkt. Tulia amewataka wabunge kutumia nafasi zao kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha kutokana na sababu inayoweza kuzuilika, wala mtoto mchanga anayefariki kwa kukosa huduma muhimu za afya.

Awali, akimkaribisha Dkt. Tulia kufungua kongamano hilo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azan Zungu, amesema Tanzania inathamini nafasi ya IPU katika kuwakutanisha wabunge na wadau mbalimbali kujadili changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya afya.


Zungu amesema kongamano hilo ni fursa muhimu kwa wabunge na wadau kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto za afya ya mama na mtoto na kutafuta suluhisho zinazoweza kutekelezwa katika nchi mbalimbali.

Amesema ushirikiano wa kibunge ni muhimu katika kuhakikisha masuala ya afya yanapewa nafasi inayostahili katika mijadala ya kisera na katika maamuzi ya kitaifa, hasa kwa kuzingatia mahitaji ya wanawake, watoto na vijana.

Spika Zungu amesema uwepo wa viongozi na wadau kutoka mataifa mbalimbali unaonyesha umuhimu wa kuunganisha nguvu katika kukabiliana na changamoto za afya zinazoikabili jamii.

Amesema kupitia majadiliano hayo, mabunge yanaweza kujifunza kutoka kwa uzoefu wa nchi nyingine, kubadilishana mbinu bora na kuimarisha hatua za pamoja zitakazosaidia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Kwa upande wake, Dkt. Tulia amewashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali, Bunge na wananchi wa Tanzania kwa kuwezesha mkutano huo na kwa ukarimu unaoendelea kuonyeshwa kwa washiriki wa mkutano wa IPU.

Amesema dhamira ya kisiasa katika kuboresha afya ya mama na mtoto ni muhimu katika kuwekeza katika maisha ya sasa na mustakabali wa mataifa, akisisitiza kuwa maendeleo katika eneo hilo yanahitaji ushirikiano wa serikali, mabunge, wataalamu wa afya na jamii kwa ujumla.

Amehitimisha kwa kuwataka wabunge duniani kuifanya ajenda hiyo kuwa utekelezaji wenye matokeo yanayopimika, ili kuhakikisha kila mwanamke, mtoto mchanga, mtoto na kijana anapata huduma muhimu za afya bila ubaguzi.



This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post