Waimarisha Ushirikiano wa Huduma za Afya Kwa Watumishi na Familia Zao
Na, Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha – Mt. Meru imeingia makubaliano na Umoja wa Afrika (African Union) kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa watumishi wa Umoja wa Afrika pamoja na familia zao watakapokuwa katika Mkoa wa Arusha.
Makubaliano hayo yanalenga kuhakikisha watumishi wa jumuiya hiyo ya kimataifa na ndugu zao wanapata huduma bora za afya wanapokuwa mkoani Arusha, hatua inayotarajiwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wageni na watumishi wa taasisi za kimataifa wanaotembelea au kufanya shughuli zao katika mkoa huo.
Aidha, Mkataba huo umesainiwa mnamo tarehe 15 Oktoba 2026, katika Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, kati ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha – Mt. Meru, Dkt. Alex Ernest, na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Afya wa Tume ya Umoja wa Afrika, Dkt. Adamu Isah (The Director of Medical and Health Services at the African Union Commission).
Hatahivyo, Makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya, huku yakifungua fursa ya kuendeleza uhusiano kati ya Hospitali ya Mt. Meru na taasisi za kimataifa. Aidha, ushirikiano huo una umuhimu kwa Taifa katika kuimarisha imani ya wadau wa kimataifa kwa huduma za afya zinazotolewa nchini Tanzania.
Kupitia makubaliano hayo, Hospitali ya Mt. Meru inaendelea kuimarisha nafasi yake katika utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia ubora, weledi na mahitaji ya wateja mbalimbali, sambamba na mchango wake katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi na wageni wanaofika katika Mkoa wa Arusha.

