Seif Mangwangi, APC Media, Arusha
Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makala amezitaka taasisi za Serikali ambazo zinahusika na miundombinu ya uwanja wa mpira wa miguu wa AFCON kuhakikisha wanashirikiana kwa pamoja Ili kuweza kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Aidha CPA Makalla amekabidhi hundi wa Bilioni2 Kwa wakazi waliokuwa wakimiliki ardhi iliyotumika kujengea uwanja huo na kusema serikali pia katika Shilingi Bilioni 340 za kutekeleza mradi huo tayari zimelipwa zaidi ya Shilingi Bilioni 200 na hivyo kumfanya Mkandarasi kutoidai serikali kwa kazi alizozifanya mpaka hivi sasa.
"Serikali haidaiwi kwa kazi zilizofanyika mpaka sasa na hii inadhihirisha dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba yeye ameweka dhamira ya Tanzania kuwa mwenyeji wa AFCON 2027 na ndio maana amekuwa akisimamia kwa karibu na kutusukuma kuhakikisha Mkandarasi analipwa kwa wakati ili kazi ikamilike kwa wakati na kwa viwango vilevile vilivyokusudiwa." Amesema Mhe. Makalla.
CPA Makala ameyasema hayo Leo 31 Disemba 2015 wakati akiongea na wakazi wa eneo linalozunguka uwanja huo akikagua maendeleo ya mradi huo ambao unatarajiwa kukamalika mapema July mwaka 2026 pamoja na kutoa hundi ya malipo ya fidia Kwa wakazi walitoa eneo Hilo kwaajili ya ujenzi wa uwanja.
Amesema kuwa taasisi kama mamlaka ya maji safi , Tarura, Tanesco,Tanroad wanatakiwa kukaa pamoja ndani ya mradi huo kila siku na endapo kama kutatokea tatizo itakuwa rahisi kulitatua kwa pamoja na kuepuka kukwamisha mradi huo kutoendelea.
"Kuanzia sasa Taasisi zote za Serikali ambazo zinahusika na mradi huu naagiza muweke kambi hapa mpaka tutakapokabidhiwa maana haiwezekani Auwsa ashindwe kutekeleza uwajibikaji wake kwa kuwa Tanesco ajatekeleza majukumu yake ipasavyo," amesema.
Mkandarasi anayejenga uwanja huo Denisi Benito amesema kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 70 na kwamba asilimia 30 zilizobaki zitakamilika baada ya baadhi ya vifaa kufika.
" mheshimiwa Mkuu wa Mkoa hadi Sasa mradi umekamilika Kwa asilimia 70, na asilimia 30 zilizobaki zinasubiria vifaa kutoka nje ya nchi, kuna umuhimu wa Serikali kuweza kuruhusu baadhi ya vifaa hasa vinavyotoka nje ya nchi kuingia kwa haraka,"amesema.
Amesema kuwa wiki chache zilizopita waliweza kuagiza chuma kutoka nje ya nchi lakini zilikaaa bandarini kwa zaidi ya siku 20 jambo ambalo lilifanya ujenzi ulikuwa ukisubiria chuma hizo kuchelewa.
Benito amesema kwa sasa vifaaa vya ujenzi vilivyobaki vinatakiwa kuingia nchini hivyo basi ni muhimu kwa Serikali mkoa wa Arusha kuhakikisha kuwa wanalisimamia hilo ipasavyo hasa taratibu za kuondoa mzigo bandarini.
RC MAKALA pia amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuchangamkia fursa za biashara, utalii pamoja na utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo Mahoteli, vyakula na usafirishaji zitakazotokana na ujenzi wa uwanja huo na ujio wa michuano ya AFCON 2027.


