TOST YATAKUWA KUPEWA MAMLAKA YA KUTATUA MIGOGORO YA KODI

Na, Egidia Vedasto, APC Media, Arusha.

Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara, Vincent Minja, amesema Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST) inapaswa kuwa na uwezo wa kutoa maamuzi yatakayotambulika na kusaidia wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kupata ufumbuzi wa changamoto zao za kikodi.

Amesema hayo katika mkutano wa usuluhishi wa malalamiko ya Kodi Jijini Arusha, mkutano uliowakutanisha wataalamu wa Kodi Duniani, ukilenga  kujenga imani na kuboresha mazingira ya biashara nchini, kwa kuwa TOST imeanzishwa mahsusi kusaidia kushughulikia malalamiko yanayohusiana na usimamizi wa kodi.

Aidha, Minja amesema malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara bado ni mengi, hali inayohitaji kuwepo kwa mfumo madhubuti na unaoeleweka wa kushughulikia changamoto hizo. Ameeleza kuwa TOST ikiwa na mfumo imara wa usuluhishi na kutoa maamuzi yanayotekelezeka, itasaidia kupunguza migogoro ya kikodi na kuwapa wafanyabiashara na wawekezaji uhakika katika kuendesha shughuli zao.

Amesema"Wafanyabiashara wote wanapaswa kufanya shughuli zao kwa kufuata taratibu rasmi, na urasimishaji wa biashara ni muhimu katika kujenga mazingira bora ya biashara na kuhakikisha kila  mfanyabiashara anatimiza wajibu wake wa kikodi"

Kwa upande wake Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Erastus Mtui, amesema jukwaa hilo limesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uhuru na mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji nchini, ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Mtui amesema mamlaka za Serikali zinapaswa kuhakikisha haki inazingatiwa katika masuala ya kodi, hususan wakati wa kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu za kodi.

 "Hatua hiyo itasaidia kujenga uaminifu kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji, pamoja na kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari.  Changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji katika masuala ya kodi zinapaswa kushughulikiwa kwa wakati kupitia mifumo ya usuluhishi iliyopo".

Minja amesisitiza kuwa TOST ipo kwa ajili ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya walipakodi, ili kuhakikisha migogoro ya kikodi inapata ufumbuzi na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Vilevile Mwenyekiti wa wafanyabiashara nchini, Kilenga Swai, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuandaa jukwaa hilo, akisema litakuwa mwarobaini wa matatizo mbalimbali ya kikodi ambayo yamekuwa yakiwakabili na kuwatesa wafanyabiashara kwa muda mrefu.


Amesema jukwaa hilo limetoa fursa kwa wafanyabiashara kueleza changamoto zao na kutafuta suluhisho la pamoja.

Swai amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara nchini, kwani itasaidia kujenga uelewano kati ya wafanyabiashara na mamlaka za Serikali. Amesema kuwa utatuzi wa changamoto za kikodi kwa njia ya majadiliano utasaidia kupunguza malalamiko na migogoro, huku ukiimarisha imani ya wafanyabiashara katika mifumo ya Serikali.

"Kipekee naipongeza Mamlaka ya Mapato na matumizi nchini  (TRA) kwa kuendelea kuboresha mfumo wake wa ukusanyaji kodi, akisema maboresho hayo yamekuwa na mchango katika kurahisisha huduma kwa walipakodi.Natoa wito kwa taasisi na mifumo mingine ya Serikali kujifunza na kuiga mfano wa TRA katika matumizi ya mifumo bora na rafiki kwa wananchi na wafanyabiashara." Amesema Swai.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post