TANZANIA YAELEZWA KUWA KINARA HUDUMA ZA AFYA AFRIKA

Na Seif Mangwangi, Arusha

Serikali imesema imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha huduma za afya nchini, ikiwa ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, kuajiri watumishi, kuimarisha miundombinu na kutekeleza sera ya bima ya afya kwa wote.

Akifungua mkutano wa pili wa kimataifa wa Afya ya msingi ( a primary Health Care Conference 2026), kwa niaba ya Rais Dr Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba Jana Jijini Arusha, amesema mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya yanaonyesha kuwa malengo yaliyowekwa na Serikali yanawezekana kutimizwa. 

Dkt Mwigulu amesema  vifo vya uzazi vimepungua kutoka takribani 328 hadi 167 kwa kila vizazi hai 100,000 katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2023, hatua ambayo alisema ni ishara ya mafanikio makubwa katika juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto.


Alisema hatua hizo pia zimeonekana katika maeneo mengine ya afya, na kwamba Serikali ya Tanzania inaamini mipango iliyowekwa itawezesha kufikia malengo ya kitaifa, kikanda na kimataifa, hususan katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu, alimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa kinara katika kusukuma mbele agenda ya afya nchini na kwamba mafanikio yote yanayoonekana ni matokeo yake. 

Alisema Rais Samia amepata heshima na tuzo mbalimbali kutokana na juhudi za Tanzania katika kuboresha afya na ustawi wa jamii.

“Mafanikio hayo si tu tuzo kwa Serikali, bali ni matokeo yanayoonekana katika maisha ya Watanzania na Waafrika kwa ujumla,lakini pia pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Tanzania na nchi nyingine za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto katika baadhi ya maeneo ya huduma za afya na hivyo ni lazima kuwe na  umuhimu wa kutumia ushahidi wa kisayansi, ubunifu na ushirikiano wa wadau ili kufikia malengo yaliyowekwa,” alisema.


Alisema hakuna njia nyingine ya kufikia malengo hayo bila kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya, na kwamba  Serikali ya Tanzania tayari imeweka afya kuwa sehemu muhimu ya mipango yake ya maendeleo.

Pia alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kujenga uwezo wa ndani badala ya kutegemea misaada kutoka nje, akisema uzoefu wa muda mrefu umeonyesha kuwa utegemezi wa misaada hauwezi kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za maendeleo.

“Tuendelee kuwekeza katika vitu vitakavyobaki na kuendelea kutusaidia,” alisema Dkt Mwigulu huku  akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika sekta zinazoweza kujenga uwezo wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi kwa muda mrefu.

Wakati huo huo, Dkt Mwigulu alisema Serikali inaendelea kusisitiza upatikanaji wa huduma za afya kwa wote bila kujali uwezo wa kipato cha mtu na kwamba moja ya njia za kufanikisha hilo ni kupitia bima ya afya kwa wote, ambayo itamwezesha mwananchi anayehitaji matibabu kupata huduma bila kikwazo cha kipato.

Alisema Serikali imeendelea kuongeza miundombinu na rasilimali watu katika sekta ya afya, sambamba na utekelezaji wa sera ya bima ya afya kwa wote.

“Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa afya, ambapo katika kipindi cha mwaka 2025/2026  imetoa ajira kwa watumishi wapya 16,000, pia inazingatia mahitaji ya wataalamu wa afya, ikiwemo madaktari na kada nyingine muhimu, pamoja na kuendelea kukamilisha miradi ya miundombinu ya afya katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.


Kwa upande wa miundombinu, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kujenga nyumba za watumishi wa afya, ambapo zaidi ya nyumba 430 zimejengwa katika maeneo mbalimbali, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya watumishi na kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.





This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post