Na, Egidia Vedasto, APC TV, Arusha.
Mkuu wa mkoa mpya wa Arusha CPA Amos Makalla ameahidi kufanya kazi na wananchi kwa kuwafuata waliko na kusikikiza kero zao akieleza kuwa hatua hiyo itawafanya wafanye kazi kwa uhuru na kuchochea uchumi wao.
Makala ametoa ahadi hiyo Leo Agosti29, 2025 wakati akikabidhiwa ofisi tayari kuanza majukumu yake mapya ya ukuu wa mkoa wa Arusha, ambapo pia amesisitiza amani na utulivu katika kipindi cha kampeni na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 29.
Makala pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kumuamini na kumpa nafasi ya kumwakilisha kutumikia wananchi wa mkoa wa Arusha na kusema atahakikisha utalii, kilimo cha mbogamboga na matunda vinakuza uchumi wa wanaarusha na taifa kwa ujumla."Naombeni tushirikiane kwa pamoja, tudumishe amani na utulivu, naijua vizuri Arusha hivyo kwa maarifa na imani yangu tutainua uchumi wetu kwa nguvu zote"
Aisha amekemea uzembe katika utendaji kazi, na kuahidi kuinua sekta ya michezo katika mkoa wa Arusha na kuzingatia misingi bora ya uongozi kama viongozi wengine waliopita.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Longido na Mwenyekiti wa wakuu wa wilaya mkoa wa Arusha Salum Khali amesema kwa umoja wao wote wameahidi kumpa ushirikiano kuhakikisha wanaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi.
"Kipaumbele chetu ni kuhakikisha tunailinda amani ya nchi yetu, na kukuza uchumi wa kila mmoja, sambamba na hayo tutahakikisha utulivu unakuwepo kipindi chote cha kampeni hadi uchaguzi" amefafanua.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru Noel Severe ameshukuru ujio wa CPA Makalla mkoani Arusha hatua itakayokuza chama na kuunganisha wananchi.
"Sisi chama cha mapinduzi tutampa ushirikiano wa kutosha katika kuhudumia wananchi na tunamshukuru Rais wetu kwa kumuamini na kumleta hapa, katika kipindi hiki muhimu katika nchi yetu kila mmoja kwa nafasi yake adumishe amani na utulivu" amesema Severe.

