NAESA YAWEKA MKAKATI KUIMARISHA HUDUMA ZA UGANI NCHINI

Na, Egidia Vedasto, APC Media, Arusha.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani za Kilimo (NAESA), Dkt. Wilhelm Mafuru amesema wakala huo umeanzishwa kwa lengo la kuratibu na kusimamia huduma za ugani nchini ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu, ushauri na teknolojia sahihi za kilimo.

Akizungumza na wakulima shambani katika Kijiji cha King'ori Wilayani Arumeru amewahakikishia wakulima kuwa  NAESA ilianzishwa kwa jukumu la kuimarisha mfumo wa huduma za ugani na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wakulima kwa ufanisi zaidi, hususan katika maeneo ya vijijini.


Dkt. Mafuru amesema miongoni mwa majukumu ya wakala huo ni kusimamia na kuratibu huduma za ugani, pamoja na kuhakikisha teknolojia na matokeo ya tafiti za kilimo yanawafikia maafisa ugani na hatimaye wakulima.

Amesema katika serikali kuhakikisha  NAESA inatimiza malengo yake, imeendelea kutoa vyombo vya moto ikiwemo pikipiki Ili Kufikia wakulima maeneo yasiyofikika kwa urahisi. 

Kwa mujibu wa Dkt. Mafuru, amesema kusogeza huduma za kitaalamu karibu na wakulima hadi ngazi za vijiji ni sehemu muhimu ya majukumu ya NAESA, kwa kuwa hatua hiyo itasaidia wakulima kupata taarifa na utaalamu kwa wakati.

Amesema huduma bora za ugani zinatarajiwa kusaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo, kupunguza upotevu wa mazao na kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao.

Dkt. Mafuru amesema NAESA inaendelea kutambulishwa katika mikoa na halmashauri mbalimbali nchini ili wadau wa sekta ya kilimo kufahamu majukumu yake na namna ya kushirikiana katika kuimarisha huduma za ugani.


Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya NAESA, Wizara ya Kilimo, TAMISEMI, taasisi za utafiti na wadau wengine wa  sekta ya kilimo, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwa wakala huo yanafikiwa na huduma bora za ugani zinawafikia wakulima nchini.

Hata hivyo amezipongeza taasisi zinazounga mkono juhudi za serikali ikiwemo BUYER katika kuinua sekta ya kilimo nchini na kuhakikisha wakulima wanatumia mbegu na dhana bora Ili walime kilimo chenye tija.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post