Na Seif Mangwangi, Arusha
SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa kuimarisha huduma za afya ya msingi ni hatua muhimu katika kuzuia na kukabiliana kwa haraka na milipuko ya magonjwa, na kusisitiza kuwa mfumo imara wa afya unaanza katika jamii kabla ya wagonjwa kufikia hospitali za rufaa.
Wito huo umetolewa Leo 9Septemba 2026, na Profesa Mohamed Janabi, akieleza kuwa uzoefu wa ugonjwa wa COVID-19 na milipuko mingine umeonesha umuhimu wa kuwa na mifumo ya afya ya msingi yenye uwezo wa kuhimili changamoto.
Akizungumza katika Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma ya Afya ya Msingi unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Mikutano Arusha AICC, Profesa Janabi alisema nchi zenye mifumo imara na inayoweza kubadilika ya afya ya msingi ziliweza kuendelea kutoa huduma muhimu wakati wa janga la COVID-19.
Amesema huduma hiyo haipaswi kuonekana kama huduma ya kiwango cha chini, bali ni huduma sahihi inayotolewa mahali sahihi na kwa wakati sahihi, kabla hali ya mgonjwa haijawa mbaya.
Profesa Janabi, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya moyo, amesema katika uzoefu wake wa kutibu wagonjwa katika vituo vya rufaa amekutana na wagonjwa wengi ambao walifika wakiwa katika hali mbaya baada ya kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Amesema baadhi yao walichelewa kupata huduma kutokana na kushindwa kumudu gharama, hali ambayo imekuwa ikimfanya kujiuliza iwapo wangepata huduma mapema katika vituo vilivyo karibu na jamii zao, huenda hali zao zisingefikia kiwango cha kuhatarisha maisha.
Aidha, amesema huduma imara ya afya ya msingi ina nafasi kubwa katika kugundua mapema magonjwa ya mlipuko na kuharakisha mwitikio wa mamlaka za afya.
Ametaja umuhimu wa kuwa na ufuatiliaji wa magonjwa katika jamii, maabara zenye uwezo, rasilimali za kutosha, ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa pamoja na hatua madhubuti za kuzuia na kudhibiti maambukizi.
Akizungumzia uzoefu wa Afrika katika kukabiliana na milipuko, Profesa Janabi amesema nchi za Rwanda na Nigeria zimeonesha mifano ya namna mifumo ya afya ya msingi inavyoweza kuimarisha upatikanaji wa huduma na kupeleka rasilimali karibu na jamii.
Amesema,Tanzania imeendelea kuonesha dhamira ya kuimarisha huduma za afya ya msingi kupitia uwekezaji katika vituo vya afya, ufadhili wa moja kwa moja wa vituo na juhudi za kupanua upatikanaji wa huduma.
Profesa Janabi aliwataka viongozi, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo kuhamisha nguvu kutoka kwenye utegemezi na miradi iliyogawanyika kwenda kwenye mifumo ya afya inayomilikiwa kitaifa na yenye uratibu madhubuti.
Amesema mkutano huo unapaswa kuzaa maazimio yenye hatua zinazopimika, majukumu yaliyo wazi na muda maalumu wa utekelezaji, badala ya kuishia katika matamko.
“COVID-19 ilituonya, mshtuko wa kifedha wa mwaka jana ulitujaribu, na mlipuko wa sasa wa Ebola unatukumbusha tena ukweli mmoja rahisi: janga halitusubiri tujenge huduma ya afya ya msingi,” amesema Profesa Janabi, na kuendelea:
“Wakati wa kutekeleza ahadi za kujenga mifumo imara ya afya ya msingi ni sasa. Afrika inahitaji ujasiri wa kufadhili huduma hizo, nidhamu ya kuzitekeleza na uwajibikaji wa kuhakikisha zinaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi,”Amesema.

