Na Egidia Vedasto,
APC Media, Arusha.
Mkuu wa mkoa Arusha Kenan Kihongosi ametoa pongezi kwa Msimamizi wa klabu ya Rotary, Mkandarasi na wadau wote waliounga mkono jitihada za ujenzi wa jengo hilo kwa viwango vya ubora katika hospitali ya Mount meru Jijini Arusha.
Akiwa katika ziara yake hospitalini hapo amesema kupatikana kwa benki ya damu salama katika hospitali hiyo itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi wakiwemo watoto, mama wajawazito na wanaopata ajali.
"Kama mnavyojua mji wetu ni wa kiutalii, jengo likikamilika itakuwa furaha yetu kubwa kuona watu wetu wanapata huduma nzuri na kwa haraka badala ya kufuata huduma ya damu katika mkoa wa Kilimanjaro, ambapo awali tulikuwa tunaenda umbali wa kilometa 80" amesema.
Hata hivyo amewataka watumishi wa hospitali ya Mount meru kupendana, kushirikiana na kutotengezeana ajali kazini.Amewakumbusha kufurahia maisha baada ya kazi ikiwemo kulala katika hoteli kubwa zilizopo Jijini humo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Klub ya Rotary katika hospitali ya Mount Meru Olais Alexander amesema mradi huo hadi kumalizika utagharimu shilingi Milioni 638 hadi kukamilika Novemba mwishoni mwaka huu.
"Kama desturi yetu ilivyo siku zote ya kusaidia jamii, na sasa tumeamua kujenga jengo la benki salama ili kuokoa maisha ya watanzania wenzetu" amesema Olais.
Vilevile msimamizi wa ujenzi wa mradi huo kutoka kampuni ya CONFIX&ENGINEERING Eng.Baraka Mkamba amesema ujenzi wa mradi umefikia asilimia 30, na juhudi zinaendelea kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kama inavyokusudiwa.
"Kwa kushirikiana na watu wa Rotary club tumeamua kuunganisha nguvu kazi kuhakikisha tunakamilisha jengo hili kwa wakati, na ifahamike kwamba ujenzi huu ni kwa ushirikiano wa wanaarusha, watanzania waishio nje na wageni wenye mapenzi mema na nchi yetu, hivyo kadri michango itakavyoendelea kuletwa tunategemea kufikia lengo mapema ili wananchi wapate huduma hii kwa wakati"ameeleza Eng. Mkamba.
Mkuu wa mkoa Kihongosi katika ziara yake ametembelea taasisi ya sayansi na teknolojia Nelson Mandera, mradi wa jengo jipya la utawala la halmashauri ya Jiji, mradi wa jengo la benki ya damu salama, kumdhamini kusikiliza kero za wananchi eneo la Soko Kuu.
Mmoja wa waliotoa kero Janeth Kileo anayefanya kazi ya kufagia barabara za jiji ameshukuru kupatiwa ufumbuzi wa changamoto yake ya kutolipwa mishahara yake kwa kipindi kirefu na ameahidiwa na Kihongosi kuwa atalipwa pesa zake zote anazodai.
