MAJONZI KWA FAMILIA, BABA AFUNGWA JELA MIAKA 23 KWA UJANGILI WA TWIGA

Maria Laban anayeishi maisha ya dhiki baada ya mume wake kufungwa jela miaka 23 kwa kosa la ujangili wa Twiga (Picha na Zulfa Mfinanga)

Na Zulfa Mfinanga, APC Blog,

Arusha.

UGUMU wa maisha ndani ya familia ni miongoni mwa changamoto inayowaathiri zaidi watoto kuliko makundi mengine ndani ya jamii.

Changamoto hiyo huathiri malezi na makuzi ya watoto ambayo ni muhimu katika kufikia ndoto zao.

Moja ya sababu inayosababisha ugumu wa maisha ni pale ambapo mzazi au mlezi kupata ugonjwa, kushuka kiuchumi au kufungwa jela.

Maria Laban (30), mkazi wa Kijiji cha Mapea, Kata ya Magugu mkoani Manyara anawakilisha kundi la wanawake Tanzania wanaolea watoto wao katika mazingira magumu baada ya mume wake Amos Bernad Mtinange kufungwa jela miaka 23 kwa kosa la ujangili wa nyama ya Twiga.

Amos alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara kwa makosa mawili ya ujangili wa Twiga pamoja na kuuza nyama ya mnyama huyo Novemba 9, 2023.

Kosa hilo lilifanyika katika ushoroba wa Kwakuchinja ambao hutumika kama mapitio na makazi ya wanyamapori katika hifadhi za Ziwa Manyara na Tarangire.

“Siku ya terehe 20/4/2023 mume wangu aliondoka nyumbani kwenda ziwani kwa ajili ya shughuli zake uvuvi.

“Siku inayofuata ya tarehe 21/04/2023 muda wa saa tisa alasiri nilipigiwa simu kuwa mume wangu amekamatwa ziwa Manyara, nikaambiwa yupo kituo cha polisi Babati, nikauliza amekatwa kwa kosa gani, nikaambiwa amekamatwa na nyara za Serikali ambayo ni nyama ya Twiga,” anasema Maria.

Maria, mama wa watoto wanne tangu kukamatwa kwa mume wake hadi kuhukumiwa, yeye na watoto wake wanaishi maisha magumu kwa kuwa mume wake ndiye aliyekuwa anategemewa kukidhi mahitaji ya familia.

 

Watoto wamekuwa kama yatima

Watoto wa Maria ni wa umri mdogo. Hulazimika kuwaacha peke yao bila uangalizi wa mtu mzima ili kwenda kutafuta vibarua mashambani, umbali wa kilometa zaidi ya 20 kutoka nyumbani.

Mtoto wa kwanza ana umri wa miaka 13, wa pili (10), wa tatu (5) na mtoto wa nne ana umri wa miaka mitatu.

“Hawa watoto wawili wanasoma, kwa hiyo mimi huwa naondoka asubuhi sana kabla hawajaenda shule, wakishaamka wanajiandaa wanaenda shule na wao huwaacha wadogo zao wenyewe, siku za mapumziko ndiyo wanashinda pamoja wote wanne.

“Kiukweli ni maisha ya hatari sana kwa watoto wangu lakini sina namna nyingine. Hebu fikiria watoto wa miaka mitano na mitatu kukaa wenyewe kuanzia saa 11 asubuhi hadi jioni, nalazimika tu kwa sababu nikisema nishinde nao tutakufa kwa njaa,” anasema Maria.

Maria alikuwa anazungumza na mwandishi wa makala haya alipomtembelea nyumbani kwake baada ya mafunzo kwa vitendo kuhusu kuripoti habari za bioanuai yaliyoandaliwa na kampuni ya Nukta Afrika kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), kupitia mradi wake wa “USAID Tuhifadhi Maliasili”

Chakula, malazi na mavazi ni mtihani

Maria anasema licha ya watoto wake kukosa ulinzi unaotakiwa lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mahitaji mengine muhimu kama vile chakula, mavazi na matibabu.

Anasema kwa sasa imekuwa ni kawaida kushindia mlo mmoja na siku chache milo miwili kwa siku ambayo kutakuwa na chakula kilicholala (kiporo).

Amos Bernad Mtinange aliyehukumiwa kifungo cha miaka 23 jela kwa kosa la ujangili wa Twiga (Picha kwa hisani ya Matukio Daima Blog)

 

 “Maisha yamebadilika sana hali ni mbaya, chakula cha watoto ni shida,” anasema Maria na kuongeza kuwa.

“Hakuna ndugu anayenisaidia toka alivyowekwa ndani hadi alivyohukumiwa. Hali hii inawaumiza sana watoto na kupelekea kuniuliza kila mara kuwa mama……hivi baba atarudi lini?…,”

Kuhusu matibabu anasema anamshukuru Mungu kwani watoto hawajaugua ingawa hajui hali itakuwaje endapo itatokea.

Maria anasema kipato chake kwa sasa ni kati ya Sh5,000 hadi Sh7,000 kwa siku na hutegemea upatikanaji wa vibarua vya mashambani.

“Kama leo tunavyozungumza sijapata kibarua kwa sababu tumekuta mashamba yamejaa maji kutokana na mvua zinazonyesha, kwa hiyo kama ningebahatika kupata kibarua usingeweza kunikuta hapa nyumbani muda huu kwa sababu huwa narudi jioni kuanzia saa 11,” anasema Maria.

Maisha ya Maria kabla ya kifungo cha mumewe

Maria anasema kabla mume wake hajafungwa maisha yalikuwa mazuri. Watoto walikuwa wanapata mahitaji yote ya msingi kwa maana ya chakula, malazi, matibabu pamoja na mahitaji ya shule.

Anasema katika kipindi hicho familia yake ilikuwa ikiishi maisha mazuri tofauti na ilivyo sasa kwa kupata mlo kamili kuanzia asubuhi hadi jioni na watoto walikuwa wanapata kifungua kinywa kabla ya kwenda shule.

 “Licha ya kuwa mume wangu ndiye aliyekuwa tegemezi wa familia lakini hata mimi mara chache nilikuwa nauza mbogamboga na samaki hapa mtaani, nilikuwa siendi mbali kwa sababu ya ulinzi wa watoto, lakini kwa sasa hilo halipo, nalazimika kwenda mbali ingawa naumia sana kuwaacha watoto wangu bila ulinzi,” anasema.

Maria anasema tangu mume wake afungwe jela hajaweza kwenda kumsalimia kutokana na ugumu wa maisha kwani upatikanaji wa pesa kwa ajili ya nauli umekuwa changamoto kwake.


Ujangili ni hatari

Sheria ya Uhifadhi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) namba 5 ya mwaka 2009 inaeleza kuwa mtu yeyote anayekutwa katika hifadhi akifanya shughuli yoyote ya kibinadamu akikamatwa atakuwa amefanya kosa la jinai na anaweza kukabiliwa na kifungo na kulipa faini kulingana na ukubwa wa kosa.

Licha ya kuwepo kwa sheria hiyo bado baadhi ya watu wanafanya kosa hilo kwa kisingizio cha kutunza familia bila kujua madhara yake.

“Hata kama mtu anafanya uhalifu huo kwa ajili ya kuendesha maisha ya familia yake, lakini anapaswa kujua maisha baada ya kufungwa jela kama ilivyo kwa Amos, sasa hivi wale watoto na mke aliyekuwa akiwatafutia wanaishije?,” anahoji Ezekiel Kyando, madau wa uhifadhi na mkazi wa Sakina jijini Arusha.

Kyando anasema amekuwa akitoa elimu kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi juu ya hasara iwapo watatumia ukaribu huo kufanya uhalifu wa wanyamapori na misitu kwamba licha ya kufungwa lakini familia zao zitaisha maisha ya mateso.

Anashauri jamii kutii sheria za uhifadhi bila shuruti kwa kufanya kazi za halali za kuwaingizia kipato ili kuepuka kuziingiza familia zao kwenye matatizo.

Twiga akiwa katika ushoroba wa Kwakuchinja (Picha na Marino Kawishe)

 

Amos alivyonaswa na askari wa uhifadhi

Kiongozi wa operesheni ya kudhibiti ujangili na uhifadhi maliasili katika ushoroba wa Kwakuchinja kutoka taasisi ya Chem chem Association, Hamis Chamkulu anasema Amos amewasumbua kwa muda mrefu hadi kukamatwa kwake.

Anasema kukamatwa kwa Amos kulitokana na mtego ulioandaliwa na askari wa uhifadhi ambao walikuwa wakifanya doria za usiku na mchana.

Amos alishatiwa nguvuni na kushtakiwa mwaka 2017 kwa kosa la ujangili, licha ya kushinda kesi hiyo bado aliendelea na ujangili bila kujua kuna kikosi cha kupambana na ujangili kinachomfuatilia kwa karibu.

“Tulipata taarifa kutoka kwenye vyanzo vyetu kuwa bado anaendelea kuua wanyama na alianza kuua wanyama wakubwa tofauti na kipindi cha nyuma alikuwa akiua wanyama wadogo,” anasema Chamkulu na kuongeza kuwa,

“Mhalifu huyu alikuwa ana mbinu za kijangili, na uwindaji wake ulikuwa ni nyakati za usiku kwa kutumia honi, pikipiki na mara nyingine alikuwa akitumia baiskeli, baada ya kubaini mbinu zake tukaweka mtego ambao ulimnasa.”

Kikosi kazi cha askari wa uhifadhi kwenye ushoroba wa Kwakuchinja kilichofanikisha kukamatwa kwa Amos (Picha kwa hisani ya Nukta Afrika)

 

Anasema msako dhidi ya Amos ulitokana na makosa mawili ya ujangili wa Twiga pamoja na kuuza nyama ya twiga ambapo siku ya tarehe 21/4/2023 walifanikiwa kumkamata kwenye kambi ya samaki kijiji cha Vilima Vitatu, ndani ya eneo la hifadhi ya jamii Burunge majira ya saa 11 jioni.

Chamkulu anasema tangu kukamatwa kwa Amos April mwaka jana hadi sasa hakuna tukio lolote la ujangili wa Twiga katika ushoroba huo.

Kikosi kazi cha kukabiliana na ujangili katika ushoroba wa Kwakuchinja kimeundwa na taasisi nne za Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), shirika lisilo kuwa la Serikali la Chem Chem Association, Burunge WMA pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Babati.


Ujangili wapungua

Takwimu za Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge zinaonyesha kuwa mwaka 2021 kulikuwa na visa nane tu vya ujangili wa wanyamapori kutoka 14 vya mwaka 2017 katika hifadhi hiyo.

Taarifa za hali ya usalama iliyotolewa Juni 2023 na Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha katika kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Aprili 2023 hakuna vifo vya wanyamapori vilivyotokana na ujangili vilivyoripotiwa Tanzania.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) hadi kufikia mwezi Aprili 2023 katika mwaka wa 2022/2023, jumla ya doria 195,912 sawa na asilimia 69 ya lengo la siku doria 284,460 zimefanyika.

Doria hizo zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa 2,786; bunduki 108; risasi 1,334; kutegua mitego 3,080 ya nyaya za kutegea wanyamapori.

Meneja Miradi kutoka Chem Chem Association, Martin Mung’ong’o anasema kwa kushirikiana na taasisi hizo nne wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja ya kutoa elimu kwa jamii juu ya uhifadhi wa maliasili, kufanya doria pamoja na kuhakikisha watuhumiwa wanapelekwa katika vyombo vya sheria.

 

 

 

 

 

 

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post