NAIBU WAZIRI MHE. KATAMBI AWASIHI WANANCHI SHINYANGA KUPUUZA WATU WANAOTUMIA RUSHWA NYAKATI ZA UCHAGUZI.

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Paschal Patrobas Katambi amewaomba wanananchi  kutowapa nafasi watu watakaoomba nafasi ya uongozi kwa njia ya rushwa.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wajasiliamali ambao umehudhuriwa na viongozi wa serikali, viongozi wa CCM pamoja na wadau mbalimbali, ambao umefanyika katika ukumbi wa ofisi za CCM Mkoa wa Shinyanga.

Mhe. Katambi amewasihi wananchi hasa wakazi wa jimbo la Shinyanga mjini kutowapa kura watu ambao hujitokeza nyakati za uchaguzi kugombea nafasi ya uongozi kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

“Tunao wajibu mkubwa sana wa kuwa na uchungu na Shinyanga yetu na kuangalia maendeleo yetu tusiwape nafasi viongozi watakaotaka madaraka kwa ajili ya maslahi yao binafsi matokeo yake wataiacha Shinyanga ikiwa hoi bila maendeleo, hii Shinyanga bila kuwa na uchungu na dhamira ya dhati ya kujitoe hatuwezi kuihudumia mimi nimeingia kwenye jimbo hili tukiwa hatuna hata uwanja wa ndege zilikuwa ni ahadi tu lakini sasa hivi uwanja ule tumepata fedha shilingi Bilioni 49 kazi inafanyika na vijana wetu lazima wapate ajila”.

“Kura yako ndiyo maendeleo yako unaweza kufurahi leo kwa kupata elifu kumi elfu ishilini lakini madhara utakayoyapata baada ya hapo ukienda Hospitali dawa hakuna vituo vya afya viko mbali, barabara mbovu hiyo laki moja yako haitakupeleka popote na watakaoumia ni watoto wetu na sisi wenyewe kwahiyo kama tutachagua viongozi kwa rushwa na fedha tutajifurahisha sisi kundi dogo lakini waliowengi wataumia nawaambia hili kwa maslahi pengine kama hutoumia wewe wahurumie watoto wako”amesema Mhe. Katambi

Aidha Mbunge Mhe. Katambi amesema ataendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wakazi wa jimbo la Shinyanga mjini huku akiwaomba kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani ili kuchochea maendeleo katika jimbo hilo.

Naibu waziri huyo  amewahakikishia wananchi kuwa suala la mikopo serikali imelifanyia kazi ambapo itaanza kutolewa Mwaka kesho 2024 baada ya  maboresho kufanyika  na kwamba Halmashauri zote zitatoa mikopo hiyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi naye amewahakikishia wananchi kuendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo ambayo imelenga kutatua kero za wananchi pamoja na kuchochea uchumi katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake naibu meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Mhe. Zamda Shaban akizungumza kwa niaba ya madiwani wa Manispaa hiyo amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano katika utatuzi wa changamoto ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono maono ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Baadhi ya wajasiliamali waliohudhuria mkutano huo wamemshukuru kwa elimu iliyotolewa huku wakimpongeza  Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Paschal Patrobas Katambi kwa kuendelea kuwajali katika mambo mbalimbali ya maendeleo.

 

Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Paschal Patrobas Katambi akizungumza kwenye mkutano huo leo Alhamis Disemba 21,2023 katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Johari Samizi akizungumza kwenye mkutano huo leo Alhamis Disemba 21,2023.  

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Child Support Tanzania akitoa elimu kwa wajasiliamali katika mkutano huo leo Alhamis Disemba 21,2023. katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.

Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga Bi. Odilia Batimayo akizungumza kwenye mkutano huo wa wajasiliamali  Alhamis Disemba 21,2023. katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Shinyanga.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post