SERIKALI YAENDELEA NA MIKAKATI YA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII

 

 Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kutekeleza  mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza, kukuza na kutangaza vivutio vya utalii nchini ikiwemo vivutio vilivyopo Kisiwa cha Ukerewe kama  Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza.Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akijibu swali  la Mbunge wa Ukerewe  Mhe. Joseph Mkundi aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa.


Amefafanua kuwa moja ya  mikakati hiyo ni pamoja na  kutangaza vivutio hivyo kwa kutumia vyombo  mbalimbali vya habari.


 "Wizara kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliratibu ziara ya kituo cha Televisheni cha ITV kwenda kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza kwa ajili ya kuandaa documentary ambayo itakapokamilika itaonyeshwa katika kipindi cha ITV cha Chetu ni Chetu" Mhe. Kitandula amesisitiza. 


 Aidha, ameongeza kuwa Wizara inaendelea kutoa mafunzo kuhusu uanzishwaji wa utalii wa utamaduni ambapo hadi sasa kuna vikundi vya utalii wa utamaduni  vikiwemo Ukerewe (Ukerewe cultural tourism Enterprises) na Nansio (Nansio cultural tourism Enterprises).


Vilevile Mhe. Kitandula amezitaka Halmashauri zote nchi kuajiri maafisa Utalii kwa ajili ya kutambua wazee wa kimila ambao ni  walinzi wakuu wa mila na tamaduni zetu.Pia Mhe. Naibu waziri amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wakati wanasubiri kupata vibali vya kuajiri maafisa utalii kuwasiliana na maafisa utalii waliopo kwenye kanda zote nchini kwa ajili ya kuwatambua wazee wa kimila na utamaduni nchini.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post