WANANCHI A.MASHARIKI WATAKIWA KUTUMIA INTERNET KUBADILI MBINU ZA KIBIASHARA

Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika jimbo la Kigamboni, Dkt Faustine Ndugulile ambaye pia ni Waziri mstaafu wa kwanza wizara ya Habari na teknolojia ya mawasiliano wa pili kutoka kulia akiwa na wazungumzaji wengine katika kikao hicho ambacho moja ya ajenda zinazozungumzwa ni pamoja na umuhimu wa mtandao wa internet katika kukuza uchumi wa wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  

 

Na Seif Mangwangi, Arusha

WANANCHI wa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki wametakiwa kuacha kufanyakazi zao kwa kutumia mbinu za kizamani na badala yake waanze kutumia njia za kisasa za kidijiti kupitia mtandao wa Internet njia ambayo imekuwa ikifikia watu wengi kwa haraka.


Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa Tisa wa Jukwaa la watumiaji wa Mtandao Afrika Mashariki unaoendelea Jijini hapa,  Msimamizi wa jukwaa hilo nchini Tanzania Nazarius Nicolaus Kirama amesema uchumi unatokana na digiti umekuwa ukikua kwa kasi katika ukanda wa Afrika Mashariki na hivyo ni wakati sasa kwa kila mfanyabiashara kuanza kutumia.


Amesema kumekuwepo na changamoto nyingi za matumizi ya Internet ambapo watumiaji wengi wamekuwa wakiweka bando kwaajili ya kuangalia mambo yasiyokuwa na faida yoyote kupitia simu zao na hivyo wanapaswa kubadilika na kuanza kutumia bando zao kwa faida.


Nazarius amesema mlipuko wa ugonjwa wa uviko 19, mbali na kusababisha vifo, pia umeleta fursa kubwa ya kiuchumi kwa wakazi wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki ambao wameweza kutumia mtandao wa Internet kujipatia kipato katika kipindi chote cha mlipuko.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela wa pili kutoka kulia, akiwa na Mbunge wa Kigamboni Dr Faustine Ndugulile wa kwanza kulia, msimamizi wa jukwaa la watumiaji wa mtandao nchini Tanzania, Nazarius Kirima wa tatu kutoka kulia na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhandisi Steven Mlote wakibadilishana mawazo mara baada ya kumaliza kufungua kongamano la watumiaji wa mtandao wa Internet     Afrika Mashariki

Amesema matumizi ya internet yamekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Afrika Mashariki tangu kuingia kwa teknolojia hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na kwamba takwimu zinaonyesha ugonjwa wa UVIKO ulivyoingia nchini, watu wengi walishindwa kufanyakazi na kubaki nyumbani na shughuli nyingi zilikuwa zikifanywa kupitia mtandao wa internet na watu wengi waliweza kutumia fursa hiyo ya mtandao kujipatia kipato.

“wakati wa ugonjwa wa UVIKO 19, biashara nyingi sana zilizokuwa zikifanywa kwa watu kukutana zilijikuta zinahamia kwenye mtandao na hapo watu wengi walibuni mbinu mbalimbali za kufanya biashara zao, hapa ndio tunaona umuhimu wa mtandao kukuza uchumi,”amesema.


Amesema katika mkutano huo washiriki watajadili namna mtandao unavyoweza kuwaingizia kipato watu wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki, lakini ni pale tu ambapo wataweza kutumia vizuri mitandao hiyo kupitia bando ambazo hununua kila siku.


Pia amesema pamoja na kuwepo kwa fursa za kiuchumi kupitia mitandao hiyo, suala la miundo mbinu pamoja na ujuzi wa matumizi ya mitandao ni mambo ambayo bado yanapaswa kujadiliwa kwa kina na kupata  majibu yake kwa haraka.

“katika mkutano huu ambao unahudhuriwa na majukwaa ya mtandao wa internet ukanda wa Afrika Mashariki utajadili mambo mbalimbali yanayokwamisha maendeleo ya Internet ikiwemo miundombinu , ushirikishwaji wa watu kidijiti na  uchumi unaotokana na digiti,”amesema.


Awali akifungua mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela kwa niaba ya Waziri wa Habari na teknolojia, Nape Nnauye, amesema Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa mtandao katika maendeleo ya nchi na kila wakati imekuwa ikiboresha sera zake na kuzifanya rafiki kwa watumiaji.


Amesema pamoja na kuwepo kwa watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii, bado mamlaka za udhibiti wa mitandao hiyo imekuwa ikihakikisha sheria na kanuni za usimamizi zinafuatwa na kuwachukulia hatua watu wanaotumia vibaya.


Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki  (Miundombinu, fedha na utawala), Mhandisi Steven Mlote amesema jumuiya hiyo imeendelea kushirikiana na majukwaa mbalimbali yanayosimamia mtandao katika ukanda wote wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuhakikisha wananchi katika nchi hizo wanafaidika kiuchumi kupitia mtandao wa internet.


This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post