Tanzania yaweka mikakati kukabiliana na tatizo la watoto wa mitaani

Katibu tawala Mkoa wa Kagera Prf Faustine Kamuzora akizungumza katika kikao hicho, katikati ni Katibu Mkuu WMJW Dr John Jingu

 Na Mwandishi Wetu WAMJW, Dodoma

IMEELEZWA kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo la kuwa na watoto wa mitaani na kwa takwimu zilizopo ni kwamba inakadiriwa kuwa na idadi ya watoto 35,919 wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika majiji na miji mbalimbali licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na Wadau kutokomeza tatizo hilo.

Hayo yamebainika wakati wa kikao kazi cha Makatibu Tawala Mikoa, Makamanda wa Polisi Mikoa na Wadau wanaohusika na masuala ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kilichofanyika leo Jijini Dodoma.

Akifungua kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema tafiti mbalimbali zimefanyika ili kubaini hali halisi ya watoto hawa mathalani “Head Count Survery” ya mwaka 2017 katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Dar es salaam ilibaini jumla ya watoto 6,393 ambao walikuwa wanaishi na kufanya kazi mtaani.

Dkt. Jingu amesema kuwa kundi hili ni kubwa na linapokuwepo katika jamii yoyote ni changamoto kwa Ustawi na Maendeleo ya Jamii husika kwani athari mojawapo ni watoto hao kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

"Kundi hili ambalo badala ya kwenda shule wanakaa Mitaani wakijilea au kulelewa na watu wasiokuwa na maadili, katika mazingira yasiyo salama na wanafanyiwa ukatili hivyo kujikuta wakijiingiza kwenye uhalifu, tatizo hili likiendelea tunatengeneza tatizo la kijamii kwa sababu kuna watu watakuwa hawajapata malezi yanayostahili" amesema Dkt. Jingu.

Ameongeza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kuweka mkakati na kuwa na mtizamo wa pamoja unaounganisha nguvu na rasilimali nyingine ili kumaliza tatizo hili kama sio kulipunguza kwa kiasi kikubwa.

Naye Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii Shilungu Ndaki akiwasilisha taarifa ya Hali ya tatizo hilo nchini amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali zinazolenga kuzuia ongezeko la watoto hawa na pia kutoa huduma ya msaada kwa watoto ambao wako tayari mtaani.

Ametaja miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na kusimamia Kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), kusimamia programu zinazolenga uchumi wa kaya na kutengeneza muongozo wa kuunganisha watoto na familia.

Ndaki amesema kwamba hadi mwezi Machi mwaka huu watoto 1005 waliokuwa mitaani wameunganishwa na wazazi wao hivyo kupunguza watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika miji na majiji.

"Changamoto kubwa pamoja na jitihada hizo watoto wameendelea kuongezeka hasa kutokana wazazi kutotimiza majukumu yao, migogoro ya ndoa na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwenye familia". ameongeza Ndaki.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la PACT Tanzania Mariana Balampama amesema kuwa, suluhisho la kudumu linahitaji ushirikiano mkubwa wa sekta mbalimbali ikiwemo kuwa na mikakati madhubuti zaidi kuzuia tatizo hilo na kubuni mbinu endelevu kwa watoto hao kwani ni sehemu muhimu kwa kizazi kijacho.

Balampama ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa Sera na mikakati inayowekwa kwa kuwashirikisha na moja ya afua muhimu inatekelezwa na Wadau ni kuwatambua, kuwarudisha na hadi sasa watoto 8003 wamefikiwa kwa miaka mitano.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Seif Shekalaghe, amesema kuna haja ya kuihamasisha jamii iache kuwapa watoto wa mitaani pesa ili kuwazuia kuongezeka hali ambayo itasaidia watoto wenye shida hasa kupatikana na kulelewa sehemu husika.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzola amesisitiza jamii kuwekeza zaidi katika malezi hasa kwa watoto wa kiume kwani inaonesha wamesahaulika na ndio idadi ya watoto wengi wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Kwa upande wa Mmiliki wa kituo cha malezi ya watoto wanaoishi mitaani cha Amani kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro Daniel Temba amesema kuwa Serikali na wadau wana jukumu la kuhakikisha watoto hasa wanaomaliza elimu ya msingi wanawekewa mazingira mazuri ya kundelea na elimu ya sekondari na hata watakaoshindwa waweze kujiunga na elimu za ufundi.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post