DC Kilosa awafunda watendaji wa kata na vijiji, *awataka kujali wananchi kwanza, kuwa na nidhamu

Na Mwandishi Wetu, Kilosa

WATENDAJI wa kata, vijiji na wenyeviti wa vitongoji wametakiwa kujituma kwa bidiii katika utekelezaji wa majukumu yao huku wakizingatia miiko ya majukumu ya kuwatumikia wananchi pamoja na kutatua changamoto za wananchi.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga alipokuwa akizungumza na watendaji hao ambapo amewataka kazi iwe ndio kipaumbele cha kwanza huku akisisitiza uwepo wa nidhamu kuanzia ngazi ya chini ya utendaji kwa kushirikiana badala ya kutunishiana misuli kwani kila mmoja yupo kisheria kwa mujibu wa majukumu yake.

Mwanga ametaka kufanyika kwa mikutano yote ya kisheria ambapo ameagiza wenyeviti wa vitongoji kuanzia Juni 1 hadi 10 kuhakikisha mikutano yote stahiki iwe imeshafanyika huku akitaka mihutasari ya vikao hivyo iwe imefika kwa watendaji wa kata ifikapo  Juni 10.

Pia  ameagiza kuwepo kwa mikutano  ya masuala ya ulinzi na usalama ambayo itakuwa ikijadili ulinzi na usalama na matukio yaliyojitokeza na namna yalivyoshughulikiwa.

"Pia nawaagiza kila eneo la utendaji kuwepo na kitabu ambacho kitakuwa kinaonyesha idadi ya wananchi waliofika ofisini na namna kero zao zilivyotatuliwa,"aliagiza.

Amewataka viongozi hao kutambua kuwa miradi yote inayofanyika katika maeneo yao inawahusu na wanapaswa kuifahamu vizuri huku upande wa elimu akiwataka viongozi hao kuhakikisha watoto wote wanaostahili kusoma wanapata haki ya kupata elimu huku akitumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji hao kuanza mapema ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekendari.

Akizungumzia migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo Alhaj Majid amewataka viongozi hao kuendelea kusimamia utii wa sheria kwa kuhakikisha usalama na amani inadumu katika maeneo yao jambo litakalosaidia  wilaya kuwa na utulivu na amani huku akitaka hatua za haraka kuchukuliwa pindi tatizo linapojitokeza ili kutoleta taharuki na hasira katikati ya jamii.

Katibu Tawala Wilaya ya Kilosa, Yohana Kasitila ametaka watendaji hao kuhakikisha miongoni mwa ajenda zinazokuwepo katika vikao vyao ni ajenda ya ulinzi na usalama, mapato na matumizi, miradi ya maendeleo na huduma za jamii.

Kaimu Meneja wa mamlaka ya mapato(TRA) Wilaya ya Kilosa, Mussa Haruni amewasihi watendaji hao kutoa ushirikiano katika kutoa hamasa kwa wananchi kulipa kodi stahiki, kutoa vitambulisho kwa watu stahiki pamoja na kuwakumbusha wananchi kudai risiti kwani kutodai risiti ni kosa kisheria. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post