WAKULIMA WA KITUNGUU MANG'OLA WALIA NA ATHARI ZA CORONA, BEI YAPOROMOKA

kitunguu kikiwa kimejazwa kwenye mifuko tayari kwa kuuzwa
Moja ya mashamba ya kitunguu katika bonde la mang'ola likiwa limevunwa

 Na Seif Mangwangi, Arusha

WAKATI Wataalam wa tiba duniani wakiendelea na harakati za kutafuta tiba ya mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Mapafu maarufu kwa jina la Corona (Covid -19), athari za ugonjwa huo zimeendelea kuonekana nchini hususani katika sekta ya Kilimo.

Wakulima wa kitunguu katika eneo la kata ya Mang’ola lililopo wilaya ya Karatu Jijini Arusha, wamesema bei ya kitunguu imeporomoka na kuwasababishia hasara kubwa tofauti na matarajio yao.

Wakizungumza na APC Blog, baadhi ya wakulima katika bonde hilo maarufu nchini kwa uzalishaji wa vitunguu vyenye ubora wa hali ya juu katika ukanda wa Afrika Mashariki walisema kuporomoka kwa bei kumesababishwa na athari za ugonjwa wa CORONA.

Walisema kuwa kutokana na ubora wa kitunguu kinachozalishwa kataka bonde hilo wanunuzi wamekuwa wakitoka katika nchi za Kenya na Uganda na ambao wamekuwa wakinunua kwa bei ya juu tofauti na mauzo ya ndani.

Wakulima hao walisema kuwa wanunuzi hao wamekuwa wakipeleka kitunguu chao hadi katika nchi za ulaya na hivyo kuwanufaisha wakulima katika bonde hilo kwa bei nzuri ya ununuzi na ambayo ilikuwa ikivutia wakulima wengi kujikita kwenye kilimo cha zao hilo.

Given Kessy ni mmoja wa  wakulima katika bonde hilo ambaye anasema kuwa tangu ugonjwa wa corona ulipoingia nchini hali ya mauzo ya kitunguu imeshuka kwa kasi kubwa kutokana na kutegemea soko la ndani ya nchi.

Amesema kuwa wakulima katika bonde hilo wamepata hasara kubwa kutokana na mauzo ya kitunguu kuwa ya bei ya chini ambayo hailingani na hali halisi ya gharama ambazo wamekuwa wakizitumia tangu kutayarisha shamba hadi kuvuna.

“ Mimi nimelima ekari moja ambapo hadi hivi sasa nimeshatumia si chini ya Tsh Milioni 6, pesa ambayo nilitegemea kuipata na faida yake baada ya kuuza kitunguu kwa faida, lakini bei zilizopo sokoni hivi sasa zinatisha, ni ndogo na haziwezi kurejesha gharama nilizotumia kulimia,”amesema Kessy.

Kwa upande wake Mkulima mwingine Emmanuel Laizer anasema kuwa tangu kulipuka kwa ugonjwa wa Corona, wakulima wa vitunguu bonde la Mang’ola wamekuwa wakipata hasara kutokana na gharama kubwa wanayoitumia kukuzia zao hilo.

“Mimi nimekuwa nikilima maeneo mbalimbali nchini, kama hapa Mang’ola na Singida, ila gharama za hapa ni kubwa sana kulinganisha na gharama za Singida, kitunguu cha hapa ni kizuri sana na kwa kawaida bei yake pia ni ya ghali, ila baada ya ugonjwa wa Corona kuibuka hali imekuwa tofauti, tumekuwa tukipata hasara tu badala ya faida,”alisema.

Alisema baadhi ya wakulima wakubwa na wenye uwezo wamekuwa wakilazimika kuvuna vitunguu vyao na kuvihifadhi kwa muda katika  maghala (store) kutokana na tatizo hilo la kushuka sana kwa bei  na kukosekana kwa wanunuzi wa vitunguu hivyo.

Laizer aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuwapatia masoko mengine nje ya nchi mbali ya Kenya na Uganda ili waweze kufidia gharama ambazo wamekuwa wakiingia wakati wa kulima zao hilo lakini pia kufanya mawasiliano na viongozi wa Kenya ili wanunuzi wa zao hilo waruhusiwe kuingia nchini kama mwanzo.

Kwa mujibu wa Laizer, bei ya gunia moja la kitunguu maarufu kama neti ya Magufuli iliyokuwa inauzwa Tsh 100,000 hadi 200,000 imeshuka na hivi sasa inauzwa kati ya Tsh 30,000 hadi 50,000 na wakati mwingine pamoja na kuwepo kwa bei hizo bado wanunuzi wanapatikana kwa tabu.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post