Vipamaru na Taswira ya maisha ya watoto kwa mataifa yaliyo bado na mfungo wa Corona.

PIX-Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vipamaru, Anania Mlalila (Kushoto)wakiwa na wadau wengine wakiwemo wanahabari katika Studio za Redio Ndingara FM wakiendesha Kipindi cha Elimu juu ya Ukatili wa kijinsia wakati wa Corona


Na Mwandishi Wetu,Mbeya.

NI jambo lisilopingika kuona kuona jambo linalofanywa na familia moja likifanywa pia na familia jirani.Hii hutokana na mfumo wa maisha wenye kuwa na mienendo yenye kufanana hata familia hizi mbili zikawa majirani.

Athari za matendo yenye kufanana kutokana na ujirani ndiyo huzidia tafsiri hata kwa watu wa mbali kutambua kuwa kwa mienendo ya mtu wa familia A ni wazi atakuwa akitokea jirani na watu wa familia B.Yawezekana ni kutokana na matendo yenye muonekano,uvaaji,matamshi,adabu,heshima na mengineyo.

Hivyo ndivyo pia ukweli usiopingika katika mwenendo wa kimaisha ulioonekana wakati wa Uonjwa wa Corona hapa Tanzania usivyoweza kutofautishwa na tafsiri inayoweza kuwa inaendelea katika mataifa jirani ambayo bado yanaendelea kusumbuliwa na ugonjwa huo wa Homa kali ya mapafu.

 

Upo uwezekano wa wadau kutoipa uzito makala haya kwakuwa Tanzania inatajwa kutokuwa tena na Corona. Lakini hatuwezi kuwaachia majirani zetu kuendelea kuzijadili athari za mlipuko huo kwakuwa makwao unatajwa kuwepo bado. Uchambuzi wetu unaweza kusaidia pia majirani kuchukua hatua madhubuti hasa kwenye kupinga ukatili dhidi ya watoto kutokana na shule kuendelea kufungwa na wao kulazimika kuwepo majumbani.

 

“Wafanyabiashara wengi wa mitaani kwa sasa wamegeuka watoto wadogo si wale watu wazima tuliowazoea na imefika mahali sehemu kama maofisini watoto hawa wamegeuka kero maana wanapoingia na biashara wanazotembeza badala ya kutamani anachokiuza unaanza kumhurumia mtoto kutokana na umri wake ikilinganishwa na kazi.”

 

“Kwa sasa tunashuhudia ukatili wa watoto unaofanywa na wazazi kuwatumikisha kazi zisizo salama.Tunaona hata kwenye vibarua vya kufyatua tofali au vya kuvuna utakuta familia nzima imebebwa hadi watoto wadogo.”

 

Hayo yalikuwa sehemu ya maneno ya Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa,Marium Kimashi kwenye mkutano wa kujadili Masuala ya Ukatili wa kijinsia na watoto katika kipindi shule zilipofungwa nchini kwaajili ya kuepuka kusambaa kwa Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.

 

Ni mkutano uliofanyika kupitia mtandao wa kijamii wa Zoom ukiandaliwa na Shirika la Vijana Pambania Maendeleo Rukwa(VIPAMARU) lenye makao yake makuu katika Manispaa ya Sumbawanga.Watoto walikuwa sehemu ya mjadala muhimu wa mkutano huu uliolenga kuyaangazia maisha yao katika kipindi walichokaa majumbani huku tarehe ya kuisha kwa likizo hiyo ikiwa haijulikani.

 

Mitazamo ya wadau katika mkutano huo ulileta taswira ya maisha halisi yaliyokuwa yakiendelea ndani ya jamii mkoani hapa.Wengi walionesha aina za ukatili walizokuwa wakifanyiwa watoto hususani wanaotoka kwenye familia duni.Wakati wenzao wakipambaniwa na wazazi na walezi wao kujisomea kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao wao walikwenda kutumikishwa,wakageuka sehemu ya nguvu kazi pasipo kujali umri wao.

 

Afisa Ufuatiliaji na Mtathimini wa Vipamaru,Donatha Haule alisema watoto wanaotokea kwenye familia zilizo na wazazi au walezi wenye ulemavu nao walikuwa na aina tofauti ya kutumikishwa.Watoto wote walitoka majumbani mwao wakiwasindikiza mjini walemavu hususani wa macho na walipofika huko watoto waligawiwa mitaa ya kuwasindikiza wakati wazazi wao wakiomba.

 

“Kwa hapa mjini tofauti na tulivyosikia kutoka maeneo mengine hapa watoto waligawiwa mitaa ya kuwatembeza wazazi wanapoomba.Huyu anaweza akaanza asubuhi saa tatu wakatembea na mlemavu labda mitaa kadhaa baadaye saa tano akachukuliwa mwingine.Hawakuwa na namna ya kujitetea wabakie nyumbani walau wajisomee au hata wajikumbushe yale waliyokwishajifunza shuleni kabla ya shule kufungwa.”alisema Dodatha.

 

Afisa Maendeleo ya jamii wa Manispaa ya Sumbawanga,Maxmillian Babile alisema ukatili dhidi ya watoto haukuishia kwenye kutumikishwa lakini pia ulibainika wa kisaikolojia ikiwemo kushuhudia ugomvi wa wazazi au walezi wao wawapo majumbani.Upo pia wa wao wenyewe kupigwa au kusemewa maneno mabaya hasa pale walipoonesha kuchoshwa na kazi walizopewa na kuhitaji kupumzika.

 

Babile alisema pia kwa watoto waliobahatika kuwa na wazazi walio na uwezo wa kuwajazia vifurushi kwenye simu zao ili waweze kujisomea na wao walijikuta wanakumbana na ukatili wa kisaikolojia.Hii ilitokea zaidi kwa watoto ambao wazazi walikosa muda wa kuwasimamia kwa karibu wakawaacha wajifanyie wenyewe mambo yao.Hawa walijikuta wanaacha kufanya kilichotarajiwa na kuanza kuingia kwenye mitandao mingine ikiwemo yenye picha zisizofaa hasa za utupu.

 

“Wazazi kwa nia nzuri wanawaachia simu watoto wao ili waweze kujisomea lakini wanapokosa usimamizi watoto wanakwenda mbali zaidi na kudownload picha za ngono.Lakini wengine wanaona kama line za mzazi zinamnyima kufanya mambo yake anaamua kutafuta kwa uficho line yake hivyo akiachiwa simu pasipo uangalizi ndiyo anayoitumia kwa mawasiliano ambayo mzazi hakunuia.”

 

Kuenezwa kwa lawama kulikokuwa kukifanywa na wanajamii ikiwemo wazazi na walezi kupiga picha watoto wao hasa walio na umri mdogo walipofanya makosa kama ya kumwaga mafuta,rangi,maji na kuzisambaza nako kulionekana kuwakera wadau wa mkutano huo wakisema ni aina ya ukatili kwakuwa umri wa watoto hao si wa kujifanyia maamuzi ya kujitangaza mitandaoni.

 

Walisema pia kupitia Sentensi za wazazi mitandaoni za Kuhoji Lini shule zitafunguliwa zikiambatana na picha za michezo ya watoto iliyokuwa inaonekana haifurahiwi na wazazi kulidhihirisha wazazi na walezi kukosa upendo kwa watoto wao.Walidhihirisha kuwa walimu wana upendo na ulezi wa kweli kwa watoto kuliko wazazi kwakuwa michezo wanayocheza nyumbani ndiyo hucheza na mashuleni chini ya walimu wao na wala walimu hawajawahi kuwapiga picha wakasambaza mitandaoni.

 “Zile picha na malalamiko ya wazazi tulianza kuyaona mitandaoni siku chache tu baada ya shule kufungwa..na imezoeleka kila kunapokuwa likizo za wanafunzi.Sasa unajiuliza wewe umekaa na mtoto wiki moja unalalamika unataka arudi shuleni mbona mwalimu anakaa naye muhula mzima na hampigi picha kuzirusha.Kumbe wenye mapenzi na watoto ni walimu na siyo sisi tunaowazaa”alisema mmoja wa washiriki mwanahabari aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Vipamaru,Anania Mlalila anasema Mkutano huo uliofanyika Juni 8 mwaka huu ulizaa matunda kutokana na maoni ya wadau hao kuleta msukumo kwa Shirika kupitia Mradi wake wa Kupinga ukatili wa Kijinsia na watoto wakati wa Covid 19 kupanua wigo wa kuyaangazia maisha ya watoto wakati shule zilipofungwa kutokana na Corona.Na sasa uangalizi huo hata baada ya Tanzania kutangazwa kutokuwepo kwa Corona unaendelezwa kila wakati wa likizo za shule.

 Matunda ya mkutano huu yakawa wadau wote walioshiriki kuwa na mkakati wa pamoja katika kuwafuatilia watoto.Kupeana taarifa mara kwa mara,kupeana mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa pasipo kujali utofauti wa kada zao za kazi.Washiriki hawa ni Uliwashirikisha Maafisa Maendeleo na Maafisa Ustawi wa jamii,Maafisa kutoka Madawati ya jinsia ya Polisi wa wilaya zote za mkoa wa Rukwa na Wanahabari.

 “Hapo ndipo tulipoamua pia kuwa na Group la WhatsApp la wadau walioshiriki mkutano huu.Lengo ni kuzidi kufanya kazi kwa ukaribu..yaani mwanahabari akipata tetesi au taarifa za Ukatili dhidi ya mtoto basi asiishie tu kuripoti bali awasiliane na Dawati la Polisi lifanye kazi yake..awasiliane na Afisa ustawi wa jamii au Maendeleo ya jamii nao walifanyie kazi.Na wakati huo huo sote tuwe tunajua nini kinachoendelea kupitia group.”

 

“Ni hapo pia tulipoona kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi mkoani hapa.Tukaanzisha mpango wa vipindi vya redio ili tusiishie sisi pekee kuwasiliana bali tuishirikishe na jamii ili na wao wawe sehemu ya washiriki katika kukemea ukatili dhidi ya watoto kwenye maeneo yao.”

 Mkurugenzi huyo anasema kumekuwepo na matokeo chanya baada ya kuanza kuendeshwa kwa vipindi vya kutoa elimu.Wanajamii wamejua aina ya ukatili wanaofanyiwa watoto katika nyakati za likizo za shule sit u wakati wa likizo ya Corona.Na pia hatua za kuchukua wanapoona mtoto wa jirani anafanyiwa ukatili zinafanyiwa kazi tofauti na awali.

 “Kupitia vipindi hivi tunapokea maoni mengi.Kwa mabinti wapo wasikilizaji walioshauri shule au vyuo zifunguliwe tu kutokana na watoto kuachwa wakizurula mitaani badala ya kubaki nyumbani kwa wakati ule.Lakini wengine wakasema baada ya shule kufunguliwa tutarajie mimba nyingi za wanafunzi.Na tayari hadi leo hii tunaambiwa kuna kesi nane za mimba kwa wanafunzi katika kata ya Lwiche manispaa ya Sumbawanga kwa mujibu wa Ripoti kutoka Polisi Dawati la jinsia katika kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu.”

 “Lakini sisi kama Vipamaru tuaamini kuwa huenda jamii iliamini kwenye matokeo mabaya ya watoto kukaa nyumbani kwakuwa hakukuwa na ushirikiano wa usimamizi wa malezi.Kila mmoja alifanya kivyake na familia yake hivyo hata alipomuona mtoto wa mwenzie akizurula alimwacha azurule.”

 Mlalila anashauri jamii kurejea katika malezi ya ushirikiano yawezekana isiwe kwa ukaribu sana kutokana na kuepuka kusambaa kwa maambukizi ya Corona lakini walau kwa kupashana habari baina ya mzazi mmoja na jirani yake pale wanapoona kuna ukakasi kwenye malezi ya mtoto uanaosababisha ukatili au mwelekeo mbovu kwakuwa kuharibikiwa kwa mtoto mmoja si hasara ya mzazi pekee bali jamii yote inayomzunguka.

 Anasema ni muhimu jamii ikatambua kuwa athari za ukatili dhidi ya mtoto ni pamoja na mhanga kukuwa katika fikra potofu za kuamini alichokuwa akifanyiwa utotoni ni halali hivyo na yeye akaja kuwafanyia watoto wake au wa jirani zake.Kuna athari pia kwa wazazi na jamii inayomzunguka wakati wa makuzi yake kwakuwa siku akikua anaweza kuamua kulipiza kisasi na ikaleta changamoto kwa jamii husika.Muhimu tahadhari zikachukuliwa mapema kwa ushirikiano.

 Baadhi ya wasikilizaji wa vipindi vya vijana na wanawake ambavyo Vipamaru wamekuwa wakivitumia kutoa elimu katika kituo cha Redio cha Ndingara FM wanasema kumekuwa na mabadiliko ya kimtazamo kwa jamii juu ya malezi ya watoto kwakuwa wanajamii wenyewe wameanza kusemana pale wanapoona jirani anakiuka miiko ya malezi ikiwemo mzazi kuendekeza ulevi na kuisahau familia yake.

Haya yaliibuliwa na Shirika la Vipamaru huko mkoani Rukwa,muhimu kwa mataifa majirani na Tanzania ni kutumia makala haya kama chachu ya kuyaangazia maisha ya watoto ambao kwenye mataifa yao wanalazimika kuendelea kuwafungia majumbani kutokana na uwepo wa Corona.Nasi watanzania wakati tukiendelea kuwaombea majirani adui huyu aondoke basi tusiache kutoa ushauri wa nini wakifanye pale tunapopata fursa kama hii.

 

 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post