Serikali yatumia Milioni 900 kukarabati Mabwawa mawili ya kunyweshea mifugo

Diwani wa Kata ya Demosileti, kijiji cha Narakauo, Wilayani Simanjiro, Mkoani Arusha, Ezekiel Senga (wa pili kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa bwawa la kunyweshea mifugo la Narakauo lililopo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara Novemba 7, 2020.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiendesha moja ya mitambo inayotumika katika ujenzi wa bwawa la Kimokuwa lililopo Wilayani Longido Mkoani Arusha alipofanya ziara ya kukagua ukarabati wa bwawa hilo
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel(kulia) akiongea na Wafugaji wa kijiji cha Narakauo, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara alipokuwa njiani kuelekea Mkoani Arusha muda mfupi baada ya kukagua ukarabati wa bwawa la kunyweshea mifugo la Narakauo Novemba 7, 2020.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Kampuni ya Ujenzi ya  Zeco, Gerald Oswald (kulia) alipofanya ziara ya kukagua ukarabati mkubwa wa bwawa la kunyweshea  mifugo la Narakauo lililopo Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara Novemba  7, 2020
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na Wafugaji na Viongozi wa Kampuni ya ujenzi ya Zeco alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa la Kimokuwa lililopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha Novemba 7, 2020.

 Na Mwandishi Wetu-Arusha


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Serikali inatumia zaidi ya shilingi Milioni 900 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa Mabwawa mawili ya kunyweshea mifugo ya Narakauo lililopo Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara na Bwawa la Kimokuwa lililopo Wilayani Longido, Mkoani Arusha.

Prof. Gabriel alieleza hayo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ukarabati wa mabwawa hayo katika Mikoa ya Arusha na Manyara Novemba 7, 2020.

Akiongea na Wafugaji wa maeneo hayo baada ya kufanya ziara hiyo, Prof. Gabriel alisema kuwa bwawa la Narakauo limetengewa milioni 413 wakati bwawa la Kimokuwa limetengewa milioni 511.9.

Prof. Gabriel alieleza kuwa ukarabati huo ni utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli alipokuwa Mkoani Manyara hivi karibuni ya kuhakikisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi inafanya jitihada za dhati kutatua changamoto ya maji kwa mifugo.

Aliongeza kuwa, mbali na ukarabati wa mabwawa hayo mawili, miradi kama hii ya ukarabati wa mabwawa ya kunyweshea mifugo unaendelea pia katika Kata ya Chamakweza, Chalinze, Mkoani Pwani na mwingine wa Kata ya Mbangala, Mkoani Songwe upo katika hatua za kukamilika, huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kuboresha upatikanaji wa maji kwa mifugo ili wafugaji waondokane na kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
 
Aidha, Prof. Gabriel alitumia nafasi hiyo pia kuitaka kampuni ya Ujenzi ya Zeco ambayo ndio imepewa jukumu la kukarabati mabwawa hayo mawili ya Narakauo na Kimokuwa kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kabla ya Novemba 25, 2020 ili kukwepa changamoto ya mvua.

“Ongezeni nguvu na spidi ya ujenzi huu ili muukamilishe kabla ya mvua hazijaanza, mvua zikiwakuta kabla hamjamaliza, kazi yote mliyoifanya itakuwa haina maana”, alisisitiza Prof. Gabriel

“Tunategemea ujenzi wa mabwawa haya uishe kwa wakati ili yaweze kusaidia wafugaji wetu ,mabwawa haya yatawapunguzia wafugaji kutembea umbali mrefu kutafuta maji”,  aliongeza Prof. Gabriel

Akizungumzia bwawa hilo, Mfugaji, kijiji cha Narakauo, Petro Narotoka aliishukuru serikali kwa kutoa pesa hizo kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo huku akiongeza kuwa mradi huo ukikamilika utakuwa ni msaada mkubwa kwa mifugo na jamii kwa ujumla.

“Ujenzi huu ukikamilika tutajitahidi sisi kama wafugaji kulinda miundo mbinu ya bwawa hili ili idumu kwa muda mrefu kwa faida ya jamii yetu”, alisema Narokota

Naye, Mfugaji wa kijiji cha Kimokuwa, Wilayani Longido, Mkoani Arusha, Kasaine Lamaiba alisema kuwa uamuzi huo wa serikali wa kujenga bwawa katika kijiji hicho umeonesha ni kwa kiasi gani serikali inathamini wafugaji nchini.

“Ujenzi wa bwawa hili utasaidia pia visima vya asili vilivyopo hapa kijijini kutumika kwa muda mrefu bila kukauka kwa sababu uwepo wa bwawa hili utaongeza chanzo cha uhakika cha maji”, alisema Lamaiba

 Aidha, prof. Gabriel aliuomba uongozi wa Halmashauri za Wilaya hizo za Longido na Simanjiro kuendelea kutoa ushirikiano ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati huku akiwaomba kuendelea kuwaandaa jamii kutunza miradi hiyo pindi itakapokamilika.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post