SERIKALI KUPITIA UPYA MIPAKA YA HIFADHI ZA TAIFA NA MAPORI TENGEFU

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hatua ambayo wizara inataka kuichukua kupima upya mipaka ya hifadhi za taifa na mapori tengefu kutokana na kuwepo kwa taarifa za baadhi ya vijiji kuvamia maeneo ya hifadhi na kuendesha shughuli za kijamii
Daniel Pius Kaimu Mkuu wa Kanda akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za kanda zilizopo njiro Jijini Arusha
Askari wa kikosi cha kulinda wanyamapori kanda ya kaskazini wakimsikiliza Naibu Waziri Constantine Kanyasu(hayuko pichani)

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI imesema iko kwenye mikakati ya kupitia na kuhakiki upya mipaka ya hifadhi za Taifa na mapori tengefu inayopakana na vijiji ili kumaliza migogoro ya mara kwa mara ambayo imekuwa ikiendelea kutokea baina ya vijiji na hifadhi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kikao kazi na wafanyakazi wa Mamlaka ya usimamizi wanyamapori kanda ya kaskazini (TAWA) katika ofisi zao zilizopo njiro jijini Arusha.

Kanyasu amesema Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikilipa fidia kubwa kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi za Taifa kutokana na kudhuriwa na wanyamapori lakini kuna taarifa kuwa wananchi katika baadhi ya vijiji ambavyo vimekuwa vikiathirika wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo kinyume cha sheria baada ya kuyavamia.

Amesema taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya mapori tengefu yamekuwa yakimegwa na vijiji vinavyozunguka na kuzuia mapito ya wanyamapori ambayo wamekuwa wakiyatumia kama njia lakini pia kuzaliana kwa baadhi ya wanyama.

Hata hivyo ameagiza viongozi wa TAWA kuhakikisha kwenye maeneo ambayo kumekuwepo na migogoro mingi ya wananchi kudhuriwa na wanyamapori kuweka kambi za kudumu ili askari wanyamapori waweze kupatikana saa zote pindi madhara yanapotokea.

“Nimeagiza  mamlaka ya TAWA iweke kambi za kudumu kwenye maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakidhuriwa mara kwa mara na wanyamapori, hii itasaidia kupunguza vifo vya wananchi lakini pia wanyama kuvamia vijiji,”amesema.

Kwa upande wake Daniel Pius Kaimu Mkuu wa Kanda, Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), amesema suala la ujangili limepungua kwa kasi kubwa katika ukanda wa Kaskazini lakini wamekuwa na changamoto kubwa ya uvamizi katika mapori tengefu kwa wananchi kuyatumia kwaajili ya kilimo.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post