TAIFA STARS BAHATI MBAYA YACHAPWA 2-1 NA LIBYA MECHI YA KUFUZU AFCON YA 2021

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA imeshindwa kulinda bao la mapema baada ya kuwaruhusu Libya kutoka nyuma kipindi cha pili na kushinda 2-1 katika mchezo wa Kundi J kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 usiku wa leo Uwanja wa Mustapha Ben Jannet mjini Monastir, Tunisia. 

Pamoja na kufungwa, Tanzania inaendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi J ikiizidi wastani wa mabao tu Libya baada ya wote kufungana kwa pointi, tatu kila timu. 

Nahodha Mbwana Ally Samatta alianza kuifungia Taifa Stars dakika ya 18 kwa mkwaju wa penalti baada ya winga Simon Happugod Msuva kuangushwa na Mohamed Aleyat kwenye boksi.
 Wakishirikiana vyema, Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji na Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco kwa pamoja na Ditram Nchimbi anayecheza Polisi kutoka Azam FC, zote za nyumbani Tanzania kwa mkopo walifanikiwa kuitia misukosuko ngome ya Libya.

Hata hivyo, tatizo likawa katika umaliziaji na kipindi cha pili pamoja na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije kuanza na mabadiliko akimtoa Salum Kimenya na kumuingiza Hassan Ramadhani ‘Kessy’ katika beki ya kulia mambo yaliharibika.

Kipa mkongwe, Juma Kaseja wa klabu ya KMC ya Dar es Salaam aliokoa mpira miguumni mwa Mohamed Soulah kwenye boksi dakika ya 53.

Sand Masaud akaisawazishia Libya kwa penalti ya utata dakika ya 68 baadaya refa  Ishmael Chizinga wa Malawi kudai beki Bakari Nondo Mwamnyeto aliunawa mpira wakati ulimgonga kwenye ugoko.

Anias Saltou akaifungia Libya bao la ushindi dakika ya 81 akimalizia pasia ya kifua ya Hamdou Elhouni kufuatia krosi ya Mofta Taktak.

Libya ikapata pigo dakika tano baadaye kufuatia Hamdou Elhouni kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Hassan Kessy.

Mechi nyingine ya kundi hilo leo, Equatorial Guinea imefungwa nyumbano 1-0 na Tunisia Uwanja wa Nuevo mjini Malabo.

Taifa Stars itarejea Tunisia Agosti 31 mwakani kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza katika kundi hilo dhidi ya wenyeji, siku ambayo Libya watakuwa wenyeji wa Equatorial Guinea.

Kikosi cha Libya kilikuwa; Ahmed Azzaqueh, Motasem Sabbou, Mohamed Aleyat, Sand Masaud, Ali Maetouq, Hamdou Elhouni, Almoatasembellah Mohamed, Mohamed Soulah/Mofta Taktak dk78, Muaid Ali/Khalid Almaryami dk62, Anias Saltou na Bader Ahmed.

Tanzania; Juma Kaseja, Salum Kimenya/Hassan Kessy dk52, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kelvin Yondan, Bakari Nondo, Muzamil Yassin, Simon Msuva, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Shaaban Iddi Chilunda dk83, Mbwana Samatta, Ditram Nchimbi na Farid Mussa/Hassan Dilunga dk68.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post