ZAIDI YA WATUHUMIWA 100 WA MAKOSA YA UHUJUMU UCHUMI WAACHIWA HURU TANZANIA

Rais wa Tanzania John Magufuli amesema zaidi ya watu 700 waliokuwa wakishutumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, ikiwemo utakatishaji wa fedha , wamekiri kutenda makosa hayo wakiomba kusamehewa, huku wengine zaidi ya 100 wakiachwa huru.
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliwataka waliotuhumiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi kukiri na kuomba radhi
Serikali ya Tanzania awali ilitoa kipindi cha siku saba ili kuandika maombi hayo, ambapo mwendesha mashtaka mkuu wa serikali alikiri kupokea mamia ya maombi kutoka kwa watuhumiwa
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli alitangaza msamaha Septemba 22, kwa watuhumiwa wa makosa hayo ambao wataandika barua za kukiri makosa, kuomba radhi na kukubali kulipa fedha wanazotuhumiwa kujipatia kinyume cha sheria.


Kuachiwa kwa washtakiwa hao kunafungamana na sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyopitishwa septemba mwaka huu inayotoa ruksa ya kufanyika mapatano baina ya watuhumiwa na mwendesha mashtaka.

Sheria hiyo inasema kuwa yeyote kati ya mtuhumiwa, wakili wake ama mwendesha mashtaka anaweza kuanzisha mapatano kwa kuiarifu mahakama.

Katika makubaliano hayo, mtuhumiwa anaweza kukiri tuhuma ama sehemu ya tuhuma dhidi yake ili kupata afueni fulani ikiwemo kuondolewa baadhi ya mashtaka,ama kupunguziwa muda ama aina ya adhabu.

Pamoja na kupokea taarifa ya wale waliokiri makosa yao, kadhalika Rais Magufuli ametoa muda mwingine wa siku saba kwa washtakiwa wengine ambao walikuwa bado hawajafikia uamuzi wa kuomba msamaha.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mashtaka ya uhujumu uchumi hayana dhamana, na wote wanaoshtakiwa kwa makosa hayo husalia rumande mpaka hukumu zao zinapotolewa.

Tangu aingie madarakani miaka minne iliyopita Rais Magufuli amekuwa akijipambanua kama kiongozi anayekabiliana na rushwa na ufisadi. Chini ya utawala wake vigogo kadhaa wameshuhudiwa wakitiwa korokoroni kwa makosa yanayohusiana na uhujumu uchumi na utakakatishaji fedha.
 Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Michael Wambura
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura ni moja ya watu maarufu ambao wanakabiliwa na mashtaka hayo, na Jumatano ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa amekwishaandika barua kwa DPP kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayomkabili mahakamani hapo na ameuomba upande wa mashtaka ufuatilie barua hiyo ili upate majibu kwa haraka.

Wambura ambaye amefungiwa maisha kujihusisha na soka, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 11 mwaka huu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 100.
CHANZO: BBC

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post