VIWANDA VINAVYOTUMIA MALIGHAFI ZA MIFUGO KUTAMBULIWA ILI KUFIKIA UCHUMI WA KATI

Na. Edward Kondela
Serikali imewataka maafisa mifugo wote nchini katika maeneo yao ya kazi kufuatilia idadi ya viwanda vinavyotumia malighafi ya mifugo ambavyo vinafanya kazi pamoja na ambavyo havifanyi kazi kufahamu changamoto  zake ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi na viwanda hivyo vianze kufanya kazi kuendana na azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo Mwaka 2025.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha hayo jana (27.10.2019) katika Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wakati alipotembelea kiwanda cha kuchakata mazao ya mifugo cha Rotiana Social Investment ambacho kwa sasa hakifanyi kazi na baadhi ya mitambo yake kuharibika na vifaa vingine kudaiwa kuibiwa na baadhi ya watu waliokuwa wakikisimamia kiwanda hicho.

Prof. Gabriel amesema lengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha inasimamia vyema azma ya serikali kuhakikisha viwanda vya malighafi za mifugo vinafanya kazi na kutaka maafisa hao wa mifugo kushirikiana na maafisa kutoka Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) katika kubaini changamoto mbalimbali zinazovikabili viwanda hivyo.

“Kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Manyara umuliki wa mitambo lazima uweze kufahamika kisheria umekaaje na kuhakikisha viwanda ambavyo vimekuwa vikichakata mazao ya mifugo vinafanya kazi ili mnyororo wa mazao ya mifugo uendelee kufanya kazi na kufikia uchumi wa kati 2025 kupitia viwanda.” Amesema Prof. Gabriel

Kuhusu kiwanda cha Rotiana Social Investment chenye eneo la Hekari 12,500 Prof. Gabriel ameutaka uongozi wa Mkoa wa Manyara kuendelea kufuatilia kwa kina umiliki wa ardhi wa eneo hilo kisheria kutokana na kiwanda hicho kutofanya kazi baada ya kuibuliwa na Taasisi ya Ilaramatak Lorkornei na Stitching Her Groen Wout ya nchini Uholanzi na kufunguliwa kiwanda mwaka 2011 ambapo kwa sasa hakifanyi kazi.

Kiwanda hicho ambacho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe zaidi ya 300 kwa siku na pamoja na mifugo mingine wakiwemo mbuzi katibu mkuu huyo ametaka pia uongozi wa Mkoa wa Manayara kufuatilia kwa kina umiliki wa mitambo hiyo kisheria na hatimaye kiwanda hicho kiweze kufanya kazi baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Bibi Mary Kisyoki ambaye amewahi kuwa mmoja wa viongozi wa Shamba la Rotiana linalomiliki kiwanda cha Rotiana Social Invetment ameshukuru uongozi wa Mkoa wa Manyara na TCCIA katika kufuatilia kiwanda hicho ambapo amesema kupitia serikali ya awamu ya tano ataendelea kusimamia ukweli ambao amekuwa akiusimamia katika kulinda mali za kiwanda hicho zinasimamiwa vyema na hatimaye kiweze kufanya kazi.

Amesema katika kipindi chote mara baada ya kiwanda hicho kusimama kufanya kazi amekuwa akihakikisha mali za kiwanda hazizidi kuibiwa au kuharibiwa na baadhi ya watu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Manyara Bibi Mwanahamisi Hussein ametoa wito kwa makatibu wenzake wa mikoa na wilaya kuzidi kutoa ushirikiano kwa serikali na sekta binafsi na kujikita kuangalia fursa na changamtoto zilizopo ili kuweza kuzitatua zikiwemo za wafugaji na kuhakikisha jamii inapata faida kutokana na yale wanayosimamia.

Aidha ameishuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweza kufuatialia masuala mbalimbali kwa kuweza kufanyia kazi yale ambayo yamekuwa yakifikishwa katika wizara hiyo likiwemo la kutofanya kazi kwa kiwanda cha Rotiana Social Investmant suala ambalo amekuwa akilisimamia ili kuhakikisha kiwanda hicho kinafahamika umiliki wake na hatimaye kiweze kufanya kazi.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post