RC MNYETI AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA GHAFLA HOSPITALI YA MBULU

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti akimpa pole mmoja kati ya wagonjwa waliokuwa wamelazwa kwenye hospitali ya Mji wa Mbulu alipofanya ziara ya ghafla.MKUU wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti katika hali isiyo ya kawaida amefanya ziara ya kushtukiza katika hospitali ya Mji wa Mbulu kwa lengo la kubaini namna wagonjwa wanavyohudumiwa. 

RC Mnyeti alifika kwenye hospitali hiyo mara mbili jana alasiri na saa tisa usiku bila uongozi wa hospitali wala wagonjwa kutambua kuwa ni mkuu wa mkoa amewatembelea ghafla. 

Awali, alifika alasiri na gari lake bila bendera na kutembelea wodi walikolazwa wagonjwa na kuzungumza nao ili kutambua namna wanavyopatiwa huduma. 

Alizungumza pia na wauguzi waliokuwepo ambapo aliwahoji namna wanavyotoa huduma ikiwemo lugha nzuri kwa wagonjwa ili wapate faraja wakati wakitibiwa. 

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Gedamar alisema lengo lake lilikuwa ni kujua namna wagonjwa wanavyohudumiwa kuliko kusubiri kuambiwa. 

“Nimefika hospitali na kukuta baadhi ya mapungufu yafanyiwe kazi, wauguzi usiku inakuwa shida kuhudumia wagonjwa, nimeshuhudia mwenyewe,” alisema Mnyeti. 

Alisema dirisha la wazee inaonyesha wameweka karatasi muda siyo mrefu baada ya kupata taarifa ya yeye kuanza ziara wilayani Mbulu. 

Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Mbulu Chelestino Mofuga alisema wanayapokea mapungufu hayo na kuhakikisha watayafanyia kazi. 
“Tunakuahidi kuwa mapungufu hayo madogo tumeyachukua na tunakuhakikishia kuwa yatafanyiwa kazi ili yasijirudie tena,” alisema Mnyeti.

Mmoja kati ya wagonjwa waliokuwa kwenye hospitali hiyo John Tsere alisema kitendo cha mkuu wa mkoa kutembelea kwa kushtukiza hospitalini hapo kitaongeza uwajibikaji kwa wauguzi na madaktari. 
“Amefika bila polisi wala viongozi wa wilaya na amevaa nguo za kawaida yaani huwezi kubaini kama ni mkuu wa mkoa wakati mwingine ni vizuri kufanya hivyo ili uone mwenyewe kuliko kusomewa taarifa,” alisema Tsere. 
Mnyeti yupo kwenye ziara ya siku nne wilayani Mbulu ya kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi na kusikiliza changamoto na kero zao ili kuyapatia majawabu. 

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post