WANAFUNZI WANAOTUHUMIWA KUMUUWA MWENZAO WARUHUSIWA KUJISOMEA WAKIWA MAGEREZA KAGERA

Na Silvia Mchuruza:
Kagera:
Kufuatia kesi ya mauaji ya mwanafunzi Mudy Muswadiku wa shule ya sekondari  Katoro Islamic Seminary  ya mkoani Kagera wanafunzi wanaotuhumiwa katika mauaji hayo wameruhusiwa kuendelea kujisomea wakiwa gerezani ili kujiandaa na mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Novemba 4, mwaka huu nchini.

Ruhusa hiyo imetolewa na mahakama baada ya Majaliwa Abdu (mwalimu) ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa katika shitaka hilo kuwasilisha maombi matatu kwa mahakama leo (Jana), kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya pili katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

Majaliwa aliiomba mahakama hati ya mashtaka pia aliomba upelelezi wa kesi hiyo uwahishwe ili kama wanafunzi hawatakuwa na hatia waweze kurudi shuleni kuendelea na masomo na kujiandaa na mitihani inayowakabili baadhi yao.

Ombi la tatu, Majaliwa aliiomba mahakama kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha nne wanaotuhumiwa katika kesi hiyo kuruhusiwa kuwa na madaftari gerezani ili waweze kuendelea kujisomea na kujiandaa na mitihani inayotarajiwa kuanza Novemba 4, mwaka huu.

Kufuatia maombi hayo, Wakili wa Serikali mkoani Kagera, Haruna Shomari alisema watuhumiwa hao watapatiwa hati hiyo ya mashtaka leo (Jana) na pia vitu kama madaftari, vitabu na kalamu wanaruhusiwa kuwa navyo gerezani.

Aliwataka wanafunzi hao wawasiliane na Mamlaka ya Magereza ili waweze kuletewa madaftari, vitabu na kalamu ili waendelee kujisomea wakiwa gerezani ili kujiandaa na mitihani hiyo.

Katika kesi hiyo pia idadi ya watuhumiwa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic ya mkoani Kagera, imeongezeka baada ya wanafunzi wengine wawili kuongezwa katika shitaka hilo. 

Wanafunzi waliongezwa ni Sharifu Amri (19) na Fahadi Abdulazizi Kamaga (20) na kusababisha idadi ya watuhumiwa kufikia wanafunzi sita, mwalimu mmoja na mlinzi mmoja wa shule hiyo.

Kesi hiyo ya mauji namba 18/2019 inayosikilizwa na Hakimu Frola Kaijage, imetajwa kwa mara ya pili leo (Jana) katika Mahakama ya Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera.

Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wanafunzi Husama Ramadhan (17), Sharifu Huled (19), Abdalah Juma (19) na Hussein Mussa (20), Majaliwa Abud (35) mwalimu na Badru Issa Tibagililwa (27) mlinzi.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Septemba 30 mwaka huu ambapo pia itatajwa tena kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza shitaka hilo.

Wakili Shomari amesema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuwa wanafunzi walioongezwa, nao wamebainika walishiriki kumpiga Mudy (marehemu).

“Katika upelelezi tunaoendelea kuifanya tulibaini kuwa pia wanafunzi hao wawili walioongezwa nao walishiriki kumpiga marehemu (Mudy) wakati huo huo bado upelelezi unaendelea,” alisema Shomari.

Mauji hayo yalitokea Aprili 14 mwaka katika shule ya sekondari ya Katoro Islamic iliyoko katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Watuhumiwa wamerudishwa rumande hadi siku kesi itakapotajwa tena.

This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post