SERIKALI YASISITIZA USHIRIKISHWAJI WA WAZAZI KUIMARISHA UNYWAJI MAZIWA SHULENI.

Na, Egidia Vedasto, APC Media, Arusha.

Wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa wamekutana Jijini Arusha kuweka mikakati ya  Kuimarisha ongezeko la unywaji maziwa katika jamii ikiwa ni  kuelekea kilele cha kitaifa cha maadhimisho ya siku ya unywaji maziwa kitakachofanyika katika septemba 30, katika viwanja vya Ngarenaro.

Akifungua kongamano hilo Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Dkt.Toba  Nguvila  amesema wazazi wanapaswa kuongeza nguvu  ya chakula hicho, kamati za shule zinapaswa kulipa kipaumbele suala hilo na kushirikiana na wadau ili kuweka mifumo endelevu ya upatikanaji wa chakula shuleni.


Amesema Maafisa Lishe, mifugo na Maafisa Elimu, wazalishaji na wasindikaji pamoja na Bodi ya Maziwa wana wajibu wa kuunganisha nguvu katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa maziwa, hasa kwa watoto na wanafunzi.

Aidha, amewataka viongozi kuhakikisha idadi ya shule zinazotekeleza mpango wa unywaji maziwa inaongezeka katika kila wilaya.

Dkt. Nguvila amesema ni muhimu kutafuta mifumo ya gharama nafuu itakayowawezesha wanafunzi kupata maziwa bora na salama kutoka kwa wafugaji na wazalishaji hadi shuleni. 

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yanapaswa kuwa kichocheo cha kujenga kizazi chenye afya na lishe bora, huku kaulimbiu ya mwaka huu, “Nyumbani, Shuleni Maziwa kwa Lishe Bora,” ikisisitiza umuhimu wa watoto kupata maziwa katika mazingira yote mawili kwa ajili ya afya, ukuaji na ustawi wao.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini, Prof. George Msalya, amesisitiza jamii kuongeza matumizi ya maziwa ili kuendana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinazopendekeza kila mtu kutumia wastani wa lita 200 za maziwa kwa mwaka.


Vilevile, amewataka wafugaji kuwa waaminifu katika maziwa wanayouza ili kulinda afya za walaji, akisisitiza umuhimu wa kutumia vifaa bora vya kuhifadhia maziwa. Amesema matumizi ya plastiki katika kuhifadhi maziwa hayafai na yanapaswa kuepukwa.

Prof. Msalya amesema unywaji wa maziwa kwa watoto una mchango mkubwa katika kujenga ubongo na kuimarisha ukuaji wao, hivyo ameiomba Serikali kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini ili kukidhi mahitaji ya jamii.

Kuhusu usalama wa maziwa, amesema yanapaswa kuchemshwa kwa kiwango kinachofaa cha joto ili kuhakikisha yanakuwa salama kwa matumizi, huku akisisitiza kuwa maziwa yaliyoharibika yanapaswa kuagwa na kutotumika.

Ameongeza kuwa uaminifu kati ya wafugaji, wazalishaji, wauzaji na walaji ni muhimu katika kuhakikisha jamii inapata maziwa salama na yenye ubora.

Katika namna hiyohiyo  Dkt. Mackrina Nombo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema elimu kwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya vijijini, bado inahitajika kuongezwa ili kutambua umuhimu wa maziwa kama sehemu ya chakula cha kila siku.

Amesema baadhi ya familia zinazofuga ng’ombe huuza maziwa yote wanayozalisha ili kupata fedha za kununua mahindi, hali inayosababisha watoto na familia hizo kukosa fursa ya kutumia maziwa kama chanzo muhimu cha lishe.

Dkt. Nombo ameeleza kuwa maziwa yana nafasi kubwa katika mwili wa binadamu na ni chakula muhimu, akibainisha kuwa katika kliniki za watoto, baadhi yao hukutwa wakiwa na uzito mdogo na kudhoofika kutokana na kutopata maziwa ya kutosha.

Pia Daktari wa mifugo kutoka halmashauri ya Wilaya Arusha vijijini Linus prosper amesema mpango wa unywaji maziwa mashuleni utasaidia Kuimarisha afya za watoto.

"Wazazi wakishirikishwa wataelewa, watachangia kama wanavyochangia chakula Kwa watoto wao".



This is received, thanks for your comments, will come back to you

Previous Post Next Post